MJEMA BLOG

JICHO LA MWANDISHI

  • RSS
  • Delicious
  • Digg
  • Facebook
  • Twitter


Daladala Moshi zagoma kutoa huduma

.F.F.U waingia mitaani kuzima vurugu

WAMILIKI na madereva wa mabasi madogo ya abiria yanayofanya safari zake katikati ya mji kama daladala na yale yanayofanya safari zake kati ya Moshi na miji jirani, wamegoma kutoa huduma kwa saa sita mfululizo.

Taarifa zinasema sababu za wamiliki na madereva hao kuamua kugoma na kuwalazimisha askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) kuingia mitaani kujaribu kudhibiti vurugu ni kupinga ongezeko la ushuru uliongezwa na Halmashauri kutoka sh1,000 hadi sh1,500 kwa siku.

Mji wa Moshi na vitongoji vyake leo ulikuwa na tafrani ya aina yake baada ya abiria wakiwamo wagonjwa kulazimika kutembea kwa miguu huku wale wenye uwezo wakilazimika kukodi pikipiki maarufu kama bodaboda.

Mgomo huo ulimalizika ulioanza saa 2:00 asubuhi ulidumu hadi saa 8:00 mchana baada ya madereva na makondakta kufikia muafaka na viongozi wa serikali wa kutazamwa upya kwa viwango hivyo vipya vya ushuru.

Mahakama yamteua Jaji Mzuna kusikiliza kesi ya Mbunge Zambi
.anadaiwa fidia ya sh2.4 bilioni na Lima Limited

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, imemteua Jaji Moses Mzuna kusikiliza kesi ya madai ya fidia ya sh2.4 bilioni inayomkabili Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi.
(Kwa habari zaidi za kina za habari hii soma Mwananchi kesho
(Background/Rejea )Kesi hiyo namba CC.7/2012 ilifunguliwa mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Moshi na kampuni ya Lima Ltd inayonunua kahawa maeneo mbalimbali nchini ikiwamo Mbozi.

Kwa mujibu wa hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani na mkurugenzi na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Lima Ltd, Eric Ng’maryo, Zambi ameisababishia kampuni hiyo hasara ya zaidi ya sh1.8 bilioni kutokana na matamshi ya kuikashifu kampuni hiyo.
Katika hati hiyo ya madai, Ng’maryo analalamika kuwa katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo Zambi ameanzisha kampeni chafu dhidi ya Lima Ltd.
“Mdaiwa ameanzisha kampeni za kuchafua kampuni yetu ili kuua ushindani ili vikundi vya wakulima anavyodai kuviwakilisha visiweze kupata ushindani”amedai Ng’maryo.
Ng’maryo ambaye ni wakili mashuhuri nchini, amedai kuwa lengo la Zambi ni kuwakandamiza wakulima wa Mbozi na mkoa wa Mbeya ili wasipate bei nzuri ya kahawa.
Msingi wa kesi hiyo ni makala iliyochapwa ukurasa wa kwanza wa gazeti la Mwanahalisi la Juni 13 hadi 19 chini ya kichwa cha habari “Mbunge CCM apinga uteuzi wa JK”.
Katika makala hiyo, Zambi amekaririwa akipinga uteuzi wa mwenyekiti mpya wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Dk. Eve Hawa Sinare na baadhi ya wajumbe wa bodi hiyo.
Ng’maryo pia ni mmoja wa wajumbe wa bodi hiyo ya wakurugenzi.
Ni katika makala hiyo mbunge huyo anadaiwa kuituhumu kampuni ya Lima Ltd yenye makao yake mjini Moshi kushawishi wakulima kuuza kahawa mbivu kwa bei ndogo sana.
Ng’maryo analalamika nukuu ya gazeti la Mwanahalisi ilitokana na barua iliyoandikwa na Zambi kwenda kwa Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Injinia Christopher Chiza.
“uhalisia na tafsiri ya kawaida ya kauli hiyo ya Zambi ni kwamba Lima Ltd ni walanguzi wanaopata faida kubwa kwa kuwanyonya wakulima wa Kahawa”amelalamika Ng’maryo.
Kutokana na kauli hizo za kashfa za Mbunge huyo, heshima ya kampuni hiyo imeshuka machoni pa wakulima na inatarajia kupata hasara ya sh600 milioni mwaka huu.
Katika kuthibitisha uhalali wa fidia hiyo, kampuni ya Lima Ltd itaegemea ushahidi kuwa Zambi ni Mbunge anayetumia nafasi yake kuanzisha vita binafsi na kampuni hiyo.
Pia kampuni hiyo itathibitisha Mbunge huyo ana maslahi katika biashara ya kahawa na anaua ushindani ili kuvipa faida vikundi vya wakulima alivyo na maslahi navyo.
“Zambi ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri lakini anafanya mambo kinyume na sheria za nchi anazopaswa kuzilinda zikiwamo kanuni zinazosimamia sekta ya kahawa”amedai.
Kampuni hiyo inaiomba Mahakama kumuamuru mbunge huyo kuilipa kampuni hiyo fidia maalumu ya sh2.4 bilioni, fidia ya fundisho, na fidia ya jumla na gharama za kesi hiyo.
Pia kampuni hiyo inaiomba mahakama kuu kutoa zuio dhidi ya Mbunge huyo wa Mbozi Mashariki kuendelea kuchapisha taarifa za kuikashifu kampuni hiyo.
mwisho

Idadi ya abiria waliofariki kwa ajali ya basi aina ya Toyota Hiace iliyokuwa ikitokea Masama kwenda Bomang'ombe wilayani Hai sasa imefikia sita baada ya abiria mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja tu la Emanuel kufariki muda mfupi uliopita.

Kwa mujibu wa Kamanda wa kikosi cha Usalama barabarani mkoa wa Kilimanjaro, Peter Simma, polisi wameanzisha msako mkali wa kumtafuta dereva wa basi hilo ambaye alitoroka kusikojulikana mara tu baada ya kutokea kwa ajali hiyo mbaya.

at Monday, June 18, 2012 Posted by Daniel Mjema 1 Comment

Watu watano wamepoteza maisha baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Masama kwenda Bomang'ombe wilayani Hai kuacha njia na kupinduka leo asubuhi saa 1:00 . Kwa taarifa za kina za habari hii soma gazeti la Mwananchi na The Citizen kesho.

at Monday, June 18, 2012 Posted by Daniel Mjema 0 Comments


KAMPUNI ya ununuzi kahawa ya Lima Limited yenye makao yake mjini Moshi, imemburuza mahakamani Mbunge wa Jimbo la Mbozi Mashariki kwa tiketi ya chama cha mapinduzi (CCM), ikimdai fidia ya shilingi bilioni 2.4.

Hata hivyo Mbunge huyo alipotafutwa na waandishi wa habari kutoa msimamoi wake juu ya kesi hiyo, alisema hajaarifiwa juu ya kuwapo kwa kesi hiyo na anasubiri akishajulishwa rasmi ndipo atajua nini cha kufanya kwa kuwashirikisha wanasheria wake.

Kesi hiyo namba 7 ya mwaka 2012 ilifunguliwa juzi katika Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Moshi na mkurugenzi wa kampuni hiyo ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya kampuni hiyo, Bw. Eric Ng’maryo.

Mbali na kuwa mwenyekiti wa bodi wa kampuni hiyo ambayo inanunua kahawa kutoka kwa wakulima katika wilaya mbalimbali nchini ikiwamo Mbozi mkoani Mbeya, pia ni mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya Bodi ya Kahawa Tanzania(TCB).

Katika kesi hiyo, Bw. Ng’maryo amedai kuwa kwa miaka mitatu sasa, mbunge huyo ameanzisha kampeni mbaya dhidi ya kampuni hiyo akiituhumu kuwa kuwalangua wakulima wa Kahawa wilayani Mbozi kwa kuwalipa bei ndogo.

Mwenyekiti huyo amedai kuwa Mbunge huyo anaendesha kampeni hizo chafu dhidi ya kampuni hiyo ili kuua ushindani wa kibiashara na hatimaye kuvipa vikundi vya wakulima alivyo na maslahi navyo, fursa ya kukusanya kahawa bila ushindani.

“kwa kufanya hivyo Mbunge huyo anakandamiza wakulima katika wilaya ya Mbozi wasipate bei nzuri ambayo ingesukumwa na kuwapo kwa ushindani katika ununuzi wa kahawa na hivyo mkulika kupata bei nzuri”amelalamika Ng’maryo.

Kutokana na matamshi hayo ya mara kwa mara ya Mbunge huyo kupitia vyombo mbalimbali vya habari, hadhi na heshima ya kampuni hiyo imeshuka miongoni mwa wakulima na kutokana na hilo inatarajia kupata hasara ya sh600,000,000 mwaka huu.

Kampuni hiyo imetolea mfano wa taarifa iliyomkariri Mbunge huyo na kuchapwa katika gazeti la Mwanahalisi la Juni 13 –Juni 19 chini ya kichwa cha habari Mbunge CCM apinga uteuzi wa JK kuwa aliingiza maneno ya kuikashifu kampuni hiyo.

Katika hati yake hiyo ya madai, kampuni hiyo imedai kuwa mbunge huyo ana maslahi binafsi katika biashara ya kahawa na amekuwa akitaka vikundi vya wakulima alivyo na maslahi navyo visipande ushindani wowote toka kwa wanunuzi wengine wa kahawa.

Kampuni hiyo imedai kuwa japokuwa Zambi ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini amekuwa akifanya mambo kinyume cha sheria ambayo anapaswa kuiheshimu ikiwa ni pamoja na kanuni zinazosimamia zao la kahawa.

Kampuni hiyo imeiomba Mahakama kumuamuru Mbunge huyo kuilipa fidia ya sh2.4 bilioni, kulipa gharama za kesi na kumzuia mbunge huyo kuendelea kuchapisha matamshi katika vyombo vya habari yanayoiikashifu kampuni hiyo.

Kesi hiyo iliyofunguliwa juzi, bado haijapangiwa Jaji atakayeisikiliza.
SIKU chache baada ya kuuawa kwa Faru wawili katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, serikali imepokea Faru wengine weusi watatu kutoka nchi Uingereza ambao watapelekwa moja kwa moja Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi mkoani Kilimanjaro.

Faru hao waliwasili jana kwa ndege kutokea nchini Uingereza na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa serikali wakiwamo wa TANAPA na kupelekwa moja kwa moja katika Hifadhi ya Mkomazi ambayo ilitangazwa hivi karibuni kuwa hifadhi.

Mwaka 2009, mradi wa Faru wa Hifadhi ya Mkomazi unaojulikana kama Mkomazi Rhino Sanctuary (MRS), ulipokea Faru wengine weusi watatu kutoka shamba la Wanyama la Dvur Kralove Zoo lililopo katika nchi ya Jamhuri ya Czechoslavakia.

Kwa mujibu wa Waziri wa maliasili, Khamisi Kagasheki kuletwa nchini kwa Faru hao kunatokana na jitihada za Mhifadhi wa Wanyama aitwaye Tony Fitzjohn anayesimamia mradi wa Faru weusi wa MRS kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa).

Hata hivyo Waziri Kagasheki alisema pamoja na jitihada hizo nzuri za marafiki wa Uhifadhi kama Tony Fitzjohn ambaye amewezesha kuletwa kwa Faru hao wawili, bado Tanzania inakabiliwa na changamoto ya ujangili.

“bado tuna tatizo la ulinzi wa Wanyamapori wetu ulinzi wetu bado sio imara kwa sababu wapo Watanzania wanaoshirikiana na majangili kuhujumu wanyama wetu na hawa ndio wanaochora michoro yote ya ujangili”alisema.

Kuletwa kwa Faru hao kumekuja siku chache baada ya Waziri Kagasheki kuwasimamisha kazi wakurugenzi wanne wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa) na Askari wanyamapori 28 kutokana na kashfa ya kuuawa kwa Faru wawili.

Faru waliouawa ni wale wanaozurura kama Wanyama wengine (free range) na walikuwa hawana vifaa vya kufuatilia nyendo zao kama walivyo Faru walioingizwa nchini kutokea Afrika Kusini maarufu kama Faru wa JK.

Kati ya Faru watano walioigharimu serikali sh7.5 bilioni walioingizwa nchini kutoka Afrika Kusini, wamebakia wanne huku mmoja akiuawa na majangili Disemba 12,2010 eneo la Nyabeho na mmoja akifa kifo cha kawaida.

Taarifa zinasema Faru anayeongeza idadi ya Faru hao wa JK kuwa wanne anatokana na miongoni mwa Faru hao watano waloletwa kutoka Afrika kusini kuzaa mtoto.

Faru hao waliopewa jina la JK kikiwa ni kifupisho cha Rais Jakaya Kikwete, wanahifadhiwa eneo la kaskazini mwa Hifadhi ya Serengeti karibu na eneo la Akiba la Gurmet wakati walioawa wapo eneo la Kusini mwa Hifadhi.

Habari zinadai tatizo la kuongezeka kwa vitendo vya ujangili ni la bara zima la Afrika ambapo kwa Afrika kusini, Faru wawili huuawa kila siku na takwimu zinaonyesha kwa mwaka jana pekee Faru 227 wameuawa nchini humo.

Mbali na kusimamishwa kazi kwa wakurugenzi wa Tanapa, lakini wiki iliyopita Waziri Kagasheki aliwasimamisha kazi vigogo wawili wa Idara ya Wanyamapori kutokana kashfa ya usafirishaji Wanyamapori hai wakiwamo Twiga kwenda Pakistan.

Waliosimamishwa kazi ni Boneventura Tarimo ambaye ni mkurugenzi msaidizi Idara ya Wanyamapori na Mohamed Madehele ambaye ni Afisa Wanyamapori mkuu wa Idara hiyo.

Mwisho

at Sunday, June 17, 2012 Posted by Daniel Mjema 1 Comment

Mtanzania Wilfred Moshi akipanda mlima Everest kwa kutumia madaraja ya chuma. Mtanzania huyo amevunja rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kupanda mlima huo hadi kileleni.

at Sunday, June 17, 2012 Posted by Daniel Mjema 0 Comments
at Sunday, June 17, 2012 Posted by Daniel Mjema 0 Comments


Mbunge CCM aburuzwa kortini

.Ni Godfrey Zambi wa Mbozi Mashariki

.Adaiwa fidia ya sh2.4 bilioni
KAMPUNI ya ununuzi kahawa ya Lima Limited yenye makao yake mjini Moshi, imemburuza mahakamani Mbunge wa Jimbo la Mbozi Mashariki kwa tiketi ya chama cha mapinduzi (CCM), ikimdai fidia ya shilingi bilioni 2.4.

Hata hivyo Mbunge huyo alipotafutwa na waandishi wa habari kutoa msimamoi wake juu ya kesi hiyo, alisema hajaarifiwa juu ya kuwapo kwa kesi hiyo na anasubiri akishajulishwa rasmi ndipo atajua nini cha kufanya kwa kuwashirikisha wanasheria wake.

Kesi hiyo namba 7 ya mwaka 2012 ilifunguliwa juzi katika Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Moshi na mkurugenzi wa kampuni hiyo ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya kampuni hiyo, Bw. Eric Ng’maryo.

Mbali na kuwa mwenyekiti wa bodi wa kampuni hiyo ambayo inanunua kahawa kutoka kwa wakulima katika wilaya mbalimbali nchini ikiwamo Mbozi mkoani Mbeya, pia ni mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya Bodi ya Kahawa Tanzania(TCB).

Katika kesi hiyo, Bw. Ng’maryo amedai kuwa kwa miaka mitatu sasa, mbunge huyo ameanzisha kampeni mbaya dhidi ya kampuni hiyo akiituhumu kuwa kuwalangua wakulima wa Kahawa wilayani Mbozi kwa kuwalipa bei ndogo.

Mwenyekiti huyo amedai kuwa Mbunge huyo anaendesha kampeni hizo chafu dhidi ya kampuni hiyo ili kuua ushindani wa kibiashara na hatimaye kuvipa vikundi vya wakulima alivyo na maslahi navyo, fursa ya kukusanya kahawa bila ushindani.

“kwa kufanya hivyo Mbunge huyo anakandamiza wakulima katika wilaya ya Mbozi wasipate bei nzuri ambayo ingesukumwa na kuwapo kwa ushindani katika ununuzi wa kahawa na hivyo mkulika kupata bei nzuri”amelalamika Ng’maryo.

Kutokana na matamshi hayo ya mara kwa mara ya Mbunge huyo kupitia vyombo mbalimbali vya habari, hadhi na heshima ya kampuni hiyo imeshuka miongoni mwa wakulima na kutokana na hilo inatarajia kupata hasara ya sh600,000,000 mwaka huu.

Kampuni hiyo imetolea mfano wa taarifa iliyomkariri Mbunge huyo na kuchapwa katika gazeti la Mwanahalisi la Juni 13 –Juni 19 chini ya kichwa cha habari Mbunge CCM apinga uteuzi wa JK kuwa aliingiza maneno ya kuikashifu kampuni hiyo.

Katika hati yake hiyo ya madai, kampuni hiyo imedai kuwa mbunge huyo ana maslahi binafsi katika biashara ya kahawa na amekuwa akitaka vikundi vya wakulima alivyo na maslahi navyo visipande ushindani wowote toka kwa wanunuzi wengine wa kahawa.

Kampuni hiyo imedai kuwa japokuwa Zambi ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini amekuwa akifanya mambo kinyume cha sheria ambayo anapaswa kuiheshimu ikiwa ni pamoja na kanuni zinazosimamia zao la kahawa.

Kampuni hiyo imeiomba Mahakama kumuamuru Mbunge huyo kuilipa fidia ya sh2.4 bilioni, kulipa gharama za kesi na kumzuia mbunge huyo kuendelea kuchapisha matamshi katika vyombo vya habari yanayoiikashifu kampuni hiyo.

Kesi hiyo iliyofunguliwa juzi, bado haijapangiwa Jaji atakayeisikiliza.


 Rais Jakaya Kikwete muda mfupi uliopita ametangaza Tume ya Katiba. Mwenyekiti ni Jaji Joseph Warioba na Makamu wake ni Jaji Augustino Ramadhani. Ina wajumbe 30 - katika mgawanyo wa nusu kwa nusu na Zanzibar- kwamba 15 kutoka Tanzania Bara na 15 kutoka Tanzania Visiwani. Katika timu hiyo wapo Profesa Mwesiga Baregu, Dk. Salim Ahmed Salim, Joseph Butiku, Dk. Sengodo Mvungi, Esther Mkwizu, Yahya Msulwa, Said El Maamry. Majina mengine yanafuata, kwani tumeipokea kwa simu ya mkononi. Tuko pamoja kwa habari za papo hapo.


watimuliwa kazi kwa kumfanya raia anywe sumu

Siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kumuamuru IGP Said Mwema kuongeza ukali ili kudhibiti nidhamu ya askari wake, Jeshi la polisi limewatimua kazi polisi wake watatu kwa tuhuma za kulidhalilisha jeshi hilo.

Waliofukuzwa kazi ni Sajenti Joseph mwenye namba D.3289 na polisi wawili wasio na vyeo PC Esebius mwenye namba F.3677 na F.6620 PC Johnson wote wa kituo cha polisi cha Tarakea wilayani Rombo.

Polisi hao wanadaiwa kula dili na mfanyabiashara mmoja wa Rombo na kisha kukamata mali za mshirika wake wa kibiashara, Genes Shayo ambaye sasa ni marehemu ni kuzipiga mnada kisha fedha kukabidhiwa mshirika wake huyo waliyekuwa wakidaiana.

Wakati wakiuza mali hizo ambazo ni magunia 50 ya maharage, polisi hao walikuwa wamemweka kizuinini mfanyabiashara huyo na walipomwachia na kugundua maharagwe yake yameuzwa aliamua kujiua kwa kunywa sumu ambayo haijajulikana hadi sasa.

at Wednesday, March 14, 2012 Posted by Daniel Mjema 0 CommentsMAUZO ya kahawa ya Tanzania iliyouzwa nje ya nchi kupitia mnada unaoendeshwa na Bodi ya kahawa Tanzania (TCB) na mauzo ya moja kwa moja nje ya nchi, yameiingizia Tanzania mapato ya karibu sh1 trilioni.

Mkurugenzi mkuu wa TCB, Adolf Kumburu alisema jana kuwa mauzo hayo ambayo ni sawa na Dola 725.2 za Marekani yalifanywa katika kipindi cha miaka sita iliyopita kuanzia msimu wa 2006/2007 hadi Februari 2012.

Katika msimu huu pekee wa kilimo wa 2011/2012 unaotarajiwa kumalizika Julai, jumla ya tani 30,000 za kahawa safi aina ya Arabica na Robusta zimekwishauza nje ya nchi na kuiingizia Tanzania sh183, 873,966,400.

Hata hivyo uzalishaji wa kahawa nchi nzima katika msimu huu unatarajiwa kushuka kulinganisha na tani 54,000 zilizozalishwa msimu uliopita wa 2010/2011. Lengo la msimu huu ni kuzalisha tani 45,000 nchi nzima.

Viwango vya mapato kwa miaka sita na misimu ya kilimo ikiwa kwenye mabano ni sh130,541,262,549 (2006/2007), sh108,731,895,971(2007/2008), sh165,947,279,905(2008/2009) na sh109,051,278,846 (2009/2010).

Katika msimu wa 2010/2011 kiasi cha sh237,729,151,800 cha fedha kilipatikana kutokana na mauzo ya kahawa na msimu huu wa 2011/2012 hadi kufikia Februari tayari Tanzania imepata mapato ya sh183.8 bilioni.

"msimu huu tuna mashaka kama tutaweza kufikia lengo la uzalishaji wa tani 45,000 kwa mwaka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo imesababisha ukame kwa baadhi ya mikoa nchini"alisema Kumburu.

Nchi za Ujerumani na Japan ndio wanunuzi wakubwa wa kahawa ya Tanzania na hivi sasa TCB imekuwa katika kampeni ya uhamasishaji soko la ndani ili unywaji wa kahawa uongezeke hadi kufikia asilimia 10.

Awali unywaji wa kahawa hapa nchini ulikuwa kati ya asilimia 1 na 2 lakini katika miaka ya hivi karibuni na mkakati wa sasa wa TCB wa uhamasishaji, umesaidia unywaji wa kahawa  kuongezeka na kufikia asilimia saba.Mmoja wa makamanada wa Chadema akiwa amevalia vazi la chama hicho likiwa na maandishi kama yanavyosomeka katika picha.
Makamanda wa Chadema toka shoto Vicent Nyerere,Mwneyekiti Freeman Mbowe,Mgombea Joshua Nassar na mwisho ni naibu katibu mkuu wa  Chadema ,Zitto Kabwe wakati wa mkutano wa ufunguzi wa kampeni za kuwania ubunge katika jimbo la Arumeru.
Kamanda Godbless Lema akizungumza na vijana mbalimbali kabla ya kuanza kwa mkutano wa kampeni katika viwanja vya liganga.
Star TV kama kawaida walikuwa LIVE kuhakikisha mkutano huo unawafikia na wengine ambao hawakuwepo katika viwanja vya Liganga.
Kamnada wa Anga ,Mh Mbowe akiwasili na choppa akiwa na mgombea Joshua Nassari  katika viwanja vya Liganga.

Umati mkubwa wa wakazi wa Arumeru wakisikiliza kwa makini hotuba toka kwa viongozi mbalimbali wa Chadema.


Utii wa Sheria bila shuruti ni kauli mbiu ambayo jeshi la polisi limeiibua hivi karibuni,inapotokea mtuhumiwa akashindwa kutii amri basi hivi ndivyo inavykuwa.

at Thursday, March 08, 2012 Posted by Daniel Mjema 0 Comments

Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe akiangalia miche mipya ya kahawa inayohimili magonjwa alipotembelea taasisi ya utafiti ya Lyamungo (TaCRI) wilayani Hai.

Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili Chuo cha Polisi mjini Moshi leo tayari kwa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi. Kulia kwake ni Waziri wa Mambo ya Ndani,Mh. Shamsi Vuai Nahodha na kushoto kwake ni Inspekta Jenerali wa Polisi,Saidi Mwema
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Chuo cha Polisi mjini Moshi .
Sehemu ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Chuo cha Polisi uliofunguliwa na Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mjini Moshi .

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUFUNGUA MKUTANO MKUU WA MWAKA WA MAAFISA WAANDAMIZI WA JESHI LA POLISI,
CHUO CHA POLISI MOSHI, TAREHE 06 MACHI 2012

Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi;
Inspekta Generali wa Polisi, Said Ally Mwema;
Mheshimiwa Leonidas Gama, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro;
Makamishna na Manaibu Makamishna wa Jeshi la Polisi;
Maofisa Wakuu wa Jeshi la Polisi;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;

Nakushukuru sana wewe Mheshimiwa Waziri pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kwa kunialika kuja kufungua Mkutano wenu. Nakupongeza kwa dhati Mkuu wa Jeshi la Polisi na viongozi wenzako kwa kuwa na utaratibu wa kukutana kila mwaka kufanya tathmini ya shughuli zenu. Huu ni utaratibu mzuri kwa vile kila Kamanda kwa ngazi yake anatoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa sera, mikakati na mipango mbalimbali ihusuyo usalama wa raia na mali zao katika eneo lake la uongozi.

Nathubutu kusema kuwa msingeweza kuwa na utaratibu mwingine mzuri kushinda huu. Matumaini yangu ni kuwa taarifa hizo zinafanya uchambuzi wa kina wa mafanikio yaliyopatikana, kasoro zilizojitokeza na changamoto mlizokabiliana nazo na mnazoendelea kukabiliana nazo. Aidha, ni matumaini yangu kuwa mjadala unakuwa wa uwazi na ukweli na kwamba hamtaoneana muhali kuambiana ukweli kuhusu kasoro za mwenzenu pale inapostahili. Ni jambo jema na la kijasiri kujiwekea utaratibu wa kujipima wenyewe.
Mheshimiwa Waziri,
Ndugu Mkuu wa Jeshi la Polisi;

Nimefurahishwa sana na Kauli Mbiu ya mkutano wenu “Usingoje, tumia rasilimali ulizonazo kuongeza ufanisi”. Ni Kauli Mbiu muafaka inayohimiza uwajibikaji na ufanisi wa kazi kwa kuzingatia rasilimali zilizopo. Inatambua hali halisi kwamba utegemee ulichonacho kutimiza majukumu yako. Usisubiri usichokuwa nacho.

Usisubiri ulichoomba au ulichoahidiwa kupata. Nawaomba mkitoka hapa mwende kwenye vituo vyenu vya kazi mkiwa mmebeba ujumbe huu mzito wa Kauli Mbiu. Mwende mkatekeleze maudhui yake kwa vitendo, kwa kushirikiana na maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali. Mkifanya hivi, bila shaka mtaweza kukidhi matarajio ya wananchi na hivyo kulinda heshima ya Jeshi letu la Polisi.

Ni ukweli ulio wazi kuwa sote tungetamani muwe na zana na vitendea kazi vilivyo bora, vingi vya kutosheleza mahitaji yetu. Lakini uwezo wa kifedha uliopo ni mdogo, vitu hivyo unavyovitaka hutavipata vyote kwa wakati mmoj. Hivyo basi hamna budi kuwa na subira, kupanga vipaumbele vyenu vizuri na hasa kuwa wabunifu ili kwa kutumia vifaa vilivyopo vizuri muweze kutekeleza majukumu yenu kwa kiwango cha kuridhisha.

Mheshimiwa Waziri;
Ndugu IGP,
Maafisa na Askari,
Nataka kuwahakikishia kuwa mimi na viongozi wenzangu Serikalini tunatambua umuhimu wa kuendelea kuliongezea Jeshi la Polisi uwezo wa kibajeti ili liweze kutimiza kwa ufanisi zaidi majukumu yake. IGP ni shahidi kwa kiasi gani tumeendelea kuongeza bajeti ya Jeshi la Polisi mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, mwaka 2005 Bajeti ilikuwa Shilingi 69 bilioni na mwaka huu wa fedha zimetengwa Shilingi 134 bilioni. Nawaahidi kuwa tutaendelea kuongeza fedha kila mwaka katika miaka ijayo. Pia tumetumia uhusiano wetu na nchi rafiki kuomba misaada inayoendelea kuimarisha Jeshi letu kwa zana, mafunzo na weledi.

Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza Maofisa, Wakaguzi na askari wote kwa kazi kubwa na nzuri muifanyayo katika kulinda maisha na mali za raia. Nawapongeza kwa uchapakazi wenu na moyo wenu wa kujitolea na kujituma. Hakika maudhui ya Kauli Mbiu yenu ya mwaka huu mmekuwa mnayatekeleza kwa vitendo. Matokeo ya jitihada zenu yanaonekana. Mafanikio ya kutia moyo yanazidi kupatikana na sote tunayashuhudia. Mwenye macho haambiwi tazama. Uhalifu (hususan wa kutumia nguvu) unaendelea kupungua nchini kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma. Kulingana na takwimu za mwaka wa jana makosa makubwa ya jinai yalipungua kutoka 94,390 mwaka 2010 hadi 76,052 mwaka 2011.

Haya ni mafanikio ya kutia moyo, lakini hamna budi mtambue kuwa bado idadi ya makosa 76,052 ni kubwa mno. Hivyo bado mnayo na tunayo kazi kubwa ya kufanya mbele yenu na yetu. Inatupasa tuongeze juhudi maradufu au hata zaidi ili tupunguze kabisa uhalifu nchini.

Ndugu Makamanda,
Maofisa Waandamizi wa Polisi;

Mheshimiwa Waziri na Inspekta Generali wamezieleza vizuri changamoto zinazolikabili Jeshi la Polisi na mimi sina haja ya kuzirudia. Napenda kutumia nafasi hii kurudia kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kusaidiana nanyi kwa kuwawezesha ili muweze kuzikabili changamoto hizo kwa mafanikio. Tumefanya hivyo miaka iliyopita, tunafanya hivyo hivi sasa na tutafanya hivyo miaka ijayo.
Tutaendelea kuliwezesha Jeshi la Polisi kifedha ili muweze kutekeleza ipasavyo majukumu yenu. Tutaendelea kuwawezesha muongeze idadi ya askari.

Tutawawezesha mpate vyombo vya usafiri, zana na vitendea kazi vya kisasa vya kufanyia kazi za kukabiliana na uhalifu. Kazi ya kulipatia Jeshi la Polisi zana na vifaa vipya vya kazi inaendelea ikiwa ni sehemu ya Programu ya Maboresho ya Jeshi la Polisi. Nawahakikishia kuwa tutaendelea kutoa fedha za kutekeleza Programu hiyo na shughuli nyingine za Jeshi la Polisi.

Tutaendelea kuwawezesha katika kuboresha mafunzo ya askari na maafisa wa Jeshi la Polisi. Natambua mahitaji ya kuviboresha vyuo vilivyopo sasa. Panapohitaji kukarabati pakarabatiwe na panapotakiwa ujenzi wa majengo mapya yajengwe. Na panapotakiwa kuanzishwa chuo kipya kianzishwe. Hatuna budi kuwekeza katika mafunzo kwani mafunzo ni msingi mzuri wa weledi na kuwa na askari wenye tabia na mwenendo mwema. Kupata zana za kisasa za upelelezi na kudhibiti uhalifu pekee hazitoshi kama zitakuwa mikononi mwa askari asiyejua kitu, asiyekuwa na nidhamu na utiifu. Kufanya hivyo kunalihakikishia Jeshi uwezo wa kutimiza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa na kuleta sifa kwa Jeshi la Polisi Tanzania.

Dunia imebadilika, Tanzania imebadilika na mbinu za uhalifu na aina za uhalifu yamebadilika. Pia, mbinu, mikakati na maarifa ya kukabiliana na uhalifu, nayo yamebadilika duniani. Lazima tusisitize mafunzo, kwani ndiyo msingi wa weledi na ufanisi. Mafunzo ndiyo njia ya kuwawezesha askari na maofisa wa Jeshi la Polisi kupata elimu na maarifa mapya kuhusu uhalifu na namna ya kukabiliana nao. Mafunzo ndiyo yatakayowezesha kuelewa zana na vifaa vipya vya kupambana na uhalifu na kujua namna ya kuvitumia. Hakuna badala ya mafunzo.

Mheshimiwa Waziri,
Ndugu Inspekta Jenerali,
Maofisa,
Wakaguzi na Askari;

Mimi na wenzangu katika Serikali tunatambua umuhimu wa kuboresha maslahi ya maofisa na askari wa Jeshi la Polisi pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kuishi. Mara baada ya kuchaguliwa mwaka 2005, nilipotembelea Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na baadhi ya kambi nilijifunza mengi kuhusu hali ya maslahi na mazingira ya kazi na malazi ya wanajeshi wetu. Baada ya hapo tulianza kuyachukulia hatua mambo hayo na tumekuwa tunaendelea kufanya hivyo hadi sasa.

Tumeboresha maslahi kwa kiasi chake na bado tunaendelea. Tumeanza ujenzi wa nyumba bora za kuishi na bado tunaendelea na mpango huo.

Napenda kurudia kuwahakikishia kuwa kwangu na wenzangu Serikalini, hakuna upungufu wa dhamira ya kuboresha na kuimarisha Jeshi la Polisi nchini kwa maana ya idadi, mafunzo, vitendea kazi, maslahi na mazingira ya kuishi. Kinachotutatiza ni uwezo wa kifedha wa Serikali ambao si mkubwa sana kuweza kumudu sawia mahitaji yote ya kugharamia shughuli zote za Serikali na Taifa. Pamoja na changamoto hizo, bado tumeendela kuthubutu kuchukua hatua na kwa haya tuliyoweza kufanya kwa upande wa Jeshi la Polisi si haba. Tunaendelea.

Mheshimiwa Waziri,
Ndugu IGP;
Sina budi kuelezea furaha yangu na pongezi za dhati kwako IGP, Makamishna walioko Makao Makuu ya Polisi pamoja na Makamanda wa ngazi mbalimbali kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na rasilimali iliyopo. Huu ni uthibitisho wa uongozi wako makini ukishirikiana na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Jeshi letu. Hakika Kauli Mbiu ya mwaka huu kwenu si jambo geni hivyo tunategemea kuona mafanikio makubwa zaidi miaka ijayo. Aidha, mnanipa moyo kuwa hapo rasilimali zitakapoongezeka Jeshi la Polisi litastawi sana.
Usalama Barabarani

Mheshimiwa Waziri,
Inspekta Generali wa Polisi,
Ndugu Makamanda;
Napenda kutumia nafasi hii kurudia maombi yangu kwenu kuimarisha usimamizi wa usalama barabarani. Ajali za barabarani zimezidi mno, hatuna budi kuzizuia zisizidi kuongezeka. Tufanye kila tuwezalo zipungue. Nawaomba mtumie fursa ya mkutano wenu huu kujadili tatizo hili kwa marefu na mapana yake na mkubaliane juu ya nini cha kufanya. Naamini mtaweza.

Nawaomba jambo hili mlipe uzito unaostahili kabla halijageuka kuwa janga la kitaifa. Ukweli kwamba katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka juzi (2010) jumla ya watu 3,687 walipoteza maisha kutokana na ajali za barabarani. Mwaka na jana (2011) katika kipindi hicho hicho idadi hiyo iliongezeka na kufikia watu 4,013. Hili si ongezeko dogo inatulazimu kushtuka na kuchukua hatua. Nafahamu dhana ya kuwianisha kuongezeka kwa ajali na kuongezeka kwa pikipiki na magari na hali ya barabara zetu. Hata hivyo hivi visiwe visingizio vya kuona kuongezeka kwa ajali za barabarani ni jambo la kawaida. Tuseme ukweli kuwa ajali nyingi zinasababishwa na uzembe wa madereva kutokuheshimu Sheria ya Usalama Barabarani na ubovu wa vyombo vya usafiri. Kwa sababu zote hizi mbili Jeshi la Polisi lina wajibu maalum kukabiliana nazo. Tafadhali timizeni ipasavyo wajibu wenu. Mkajipange vizuri, kwa kushirikiana na Idara nyingine husika za Serikali, ili ajali na vifo viweze kupungua.
Madereva wazembe, walevi na wasiotaka kufuata Sheria na Kanuni za usalama barabarani wachukuliwe hatua kali. Wakati umefika madereva wakaidi wanyang’anywe leseni zao ili wasihatarishe tena maisha ya Watanzania. Najua haiwezekani kukomesha kabisa ajali za barabarani, lakini naamini kuzipunguza inawezekana. Endapo kuna msaada mnahitaji au jambo mnataka kutoka kwetu, tuambieni. Kama mnadhani Sheria ya Usalama Barabarani na Kanuni zake zinahitaji marekebisho, tuleteeni mapendekezo yenu tuyafanyie kazi. Au kama mnaona kuna mapungufu katika mfumo wa kitaasisi uliopo, msisite kutushauri na sisi tutaangalia namna ya kurekebisha.

Mheshimiwa Waziri,
Ndugu IGP,
Makamanda, Maafisa na Askari,
Jambo lingine ninalopenda mlizungumze kwa kina na mkubaliane katika Jeshi letu ni juu ya hatua za kuchukua dhidi ya tuhuma za kuenea kwa vitendo vya rushwa katika Jeshi la Polisi. Najua mnajitahidi lakini bado ni hisia ya muda mrefu ya wananchi na haionekani kubadilika. Utafiti unaofanywa na taasisi zinazojihusisha na masuala ya utawala bora kuhusu rushwa bado zinalinyooshea kidole chombo chetu hiki muhimu sana cha dola. Natamani sana hisia na taarifa hizo ingekuwa hazina chembe ya ukweli lakini, bahati mbaya huo ndio mtazamo wa jamii na inaelezea wakati mwingine kwa nini baadhi ya wananchi huchukua sheria mikononi mwao.

Pamoja na kuwepo kwa hisia hizo mimi naamini wapo Polisi wengi wazuri na kwamba hali haijafikia kusema imeshindikana kupambana na kukomesha vitendo vya rushwa katika Jeshi la Polisi. Penye nia pana njia. Tafadhali sana tieni nia ya dhati kupambana na tatizo hili na kushinda. Watambueni wale wenzenu miongoni mwenu wenye tabia ya kuomba kitu kidogo muwawajibishe ipasavyo kwa adhabu zinazostahili. Hawa ni watu wanaosaidia wahalifu wasibanwe na mkono wa sheria hivyo ni kikwazo kwa Jeshi la Polisi kutimiza ipasavyo wajibu wake wa msingi wa kupambana na uhalifu. Waondoeni katika Jeshi kwani wanaharibu sifa yenu nzuri na kudhoofisha Chombo chetu.

Mheshimiwa Waziri,
Ndugu IGP,
Ndugu Makamishna,
Maofisa Waandamizi wa Polisi;
Mabibi na Mabwana;
Yamekuwapo malalamiko mengi ya ukiukwaji wa haki za binadamu yanayoelekezwa kwa Jeshi letu la Polisi katika utendaji kazi. Taarifa za kila mwaka zinazotolewa na Tume ya Haki za Binadamu na taasisi nyingine mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa zimekuwa zikionesha hivyo. Yapo pia madai ya watu kunyanyaswa na Polisi kwa kukamatwa bila makosa, kubambikiwa makosa, kuteswa wakiwa mahabusu na hata kuuliwa. Kuna madai ya Polisi kutumia nguvu kupita kiasi na hata kusababisha vifo ya raia.

Nawaomba mtumie fursa ya mkutano huu myazungumze madai hayo na kuamua hatua zipasazo za kuchukua. Natambua kuwa katika Programu ya Maboresho ya Jeshi kuwaelimisha wanajeshi wetu kuhusu masuala ya haki za binadamu ni moja ya mambo yaliyopewa kipaumbele. Nawaomba mtekeleze dhamira yenu hii njema kwa kasi zaidi ili katika kipindi kifupi muwafikie Polisi wetu wote. Aidha, mafunzo kuhusu haki za binadamu yawemo katika mitaala ya vyuo vyetu hapa CCP, Police College – Kurasini na Chuo cha Maafisa Wakuu Kidatu.

Aidha, Jeshi liweke utaratibu mzuri na unaoeleweka wa kupokea na kufanyia kazi malalamiko au maoni yanayopelekwa kwao na wananchi.

Ni muhimu kwa Jeshi la Polisi kusisitiza na kusimamia kwa dhati nidhamu ya maofisa na askari wake. Nidhamu ni sifa ya msingi ya askari. Askari asiye na nidhamu amepoteza sifa ya kuendelea kuwa mwanajeshi. Ni hatari sana kwa usalama wa raia na anaharibu sifa ya Jeshi. Vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyofanywa na baadhi ya maofisa na askari kamwe visivumiliwe. Hivi majuzi nimesikia kuwa hapa Moshi askari ametoroka lindo na kwenda disco, tena akiwa na silaha! Vitendo vya namna hii vinaleta fedheha kwa Jeshi la Polisi na kuwaacha watu wakishangaa na kuwa na maswali mengi juu ya Jeshi lao. Inawezekanaje ifikie hapo kwa askari aliyefunzwa vizuri.

Nawaomba mzingatie upya taratibu zenu za ajira. Wakati umefika wa kuwepo na utaratibu mzuri wa upekuzi wa vijana kabla ya kuteuliwa kusomea kazi ya Polisi. Pawepo na utaratibu thabiti na kufuatilia mienendo ya askari wakati wote wa utumishi wao. Majeshi mengine yanafanya hivyo. Kufanya hivyo kutasaidia kupata vijana walio safi kwa tabia na mwenendo kuajiriwa na kuendelea na utumishi katika Jeshi la Polisi. Kwa ajili hiyo tutakuwa na askari walio watiifu, waaminifu, wachapa kazi hodari na kuliletea sifa Jeshi letu.

Mwisho

Mheshimiwa Waziri,
Inspekta Generali,
Makamanda wa Polisi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu napenda kurudia kutoa pongezi za dhati kwa kazi kubwa na nzuri muifanyayo pamoja na changamoto mbalimbali mnazokabiliana nazo. Nawapongeza sana kwa kubuni utaratibu wa Polisi Jamii ambao ni mfano mzuri wa ubunifu wa kutumia rasilimali zilizopo. Tafadhali uimarisheni na kuuboresha utaratibu huu mzuri. Sisi katika Serikali tutafanya kila linalowezekana kuongeza rasilimali kwa Jeshi la Polisi ili kuliwezesha kukabiliana na uhalifu nchini. Nawaomba mkumbuke na kuzingatia ukweli kwamba katika kila hatua mnayopiga, sisi Serikalini na taifa zima kwa ujumla tutakuwa pamoja nanyi kuwapa moyo na kuwaunga mkono kwa rasilimali muhimu.

Ndugu Inspekta Jenerali,
Makamanda wa Mikoa na Vikosi,
Mabibi na Mabwana,
Baada ya kusema hayo, ninayo furaha sasa kutamka kwamba, Mkutano Mkuu wa Mwaka 2012 wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi umefunguliwa rasmi. Nawatakia mkutano mwema, mazungumzo yenye ufanisi na matokeo mazuri.

“Ahsanteni kwa kunisikiliza”

Polisi aliyetinga katika ukumbi wa pub alberto akiwa na bunduki aina ya smg yenye risasi 30 ametimuliwa kazi .

Kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro Absalomu Mwakyoma  alisema polisi huyo amefukuzwa kazi baada ya kupatikana na hatia katika mahakama ya kijeshi iliyoketi ijumaa.


“Amefukuzwa kazi kwa fedheha kutokana na  kutenda mambo ambayo ni kinyume na mwenendo mwema”alisema Mwakyoma.

 Wiki iliyopita polisi huyo alitoroka lindo  kisha kwenda klabu ya usiku mjini Moshi akiwa na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG) usiku .

Kitendo hicho kilisababisha mtafaruku katika klabu ya Pub Alberto baada ya meneja wa klabu hiyo kumkuta askari huyo akiingia ndani kupitia lango kubwa usiku wa manane, akiwa na silaha hiyo ya kivita.

Meneja wa ukumbi huo, Thadeus Kimaro alisema alikutana na polisi huyo akiwa na bunduki hiyo aina ya SMG akitaka kuingia ukumbini humo kupitia lango kuu, kwa kuwa mlango wa kuingilia wateja tayari ulikuwa umefungwa.

“Wakati natokea Cool bar muda wa saa 9:00 usiku, nilikutana na mtu aliyetaka kuingia na bunduki huku akitweta na akisema kuna mtu amemuudhi ndani na alitaka kumuonyesha,”alisimulia  Kimaro.

Meneja huyo alisema wakati huo tayari muda wa kuingia wateja ulikuwa umepita na hivyo, mlango kufungwa na kuachwa lango kuu ili wateja waliobaki watoke.

Taarifa zaidi zilisema  askari huyo aliyekuwa katika lindo kwenye kituo kikuu cha mkoa, aliondoka lindoni akiwa na silaha hiyo iliyokuwa na risasi 30 ndani yake.

Inadaiwa kuwa awali polisi huyo alifika eneo la klabu hiyo akiwa kwenye gari binafsi na alikuwa ameongozana na wenzake watatu, lakini kabla ya kuingia ukumbini alibadili sare za kazi na kuziacha kwenye gari pamoja na silaha.

Muda kidogo baada ya kuingia ndani, alilikorofishana na mmoja wa watu waliokuwa ukumbini hapo, hivyo kuamua kwenda kwenye gari kuchukua silaha kwa malengo ambayo hayakufahamika mara moja, lakini alikutana na meneja huyo akiwa na walinzi ambao walimzuia asiingie ndani.

Meneja huyo alisema, akishirikiana na walinzi, walimsihi na kumwelewesha kuwa isingekuwa vyema kuingia na silaha kwa kuwa haziruhusiwi ndani ya ukumbi.  Aliridhika kwa shingo upande na kurudisha silaha kwenye gari.

"Kama angefanikiwa kuingia ndani ya ukumbi na silaha hiyo nahisi maafa yangekuwa ni makubwa, kwa kuwa kwa uelewa wangu SMG inabeba risasi 30," alisema Meneja huyo.
 

at Tuesday, March 06, 2012 Posted by Daniel Mjema 0 Comments

Wananchi mbalimbali wa mji wa Moshi wamepanga kufanya maandamano makubwa kupinga hatua ya Tanesco kupinga kuendesha mgawo wa saa kati ya 10 na 12 bila kutoa maelezo yeyote.

Wakizungumza na blog ya MJEMADANI wananchi hao wameadai kuchoshwa na ubabaushaji huo wa Tanesco ambao haujali dhana ya mteja ni mfalme na badala yake umeme hukatwa bila maelezo yoyote.

Mmoja wa wanaharakati anayeratibu maandamano hayo Danny Njau amesema Kesho watawasilisha barua polisi ya kumba kibali cha maandamano hayo.

"Tunataka Tanesco wafike mahala wanawajibika kutoa notisi kwa kukata umeme kwa wateja wao wanapokuwa na ulazima wa kukata Umeme.sio kujikatia umeme kana kwamba wanao wahudumia ni Ng'ombe wasio stahili haki ya kujulishwa"alisema Njau.

at Tuesday, March 06, 2012 Posted by Daniel Mjema 0 Comments
Rais Jakaya Kikwete akiwa na wapandaji mlima kutoka nchini Botwana. 


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na waziri wa maendeleo ya jamii jinsia na watoto, Sophia M. Simba, Msaidizi wa katibu mkuu wa umoja wa mataifa , Mr. John Hendra, First Lady Mama Salma Kikwete na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama wakiungana na wapandaji mlima 90 wa kiume na kike kutoka mataifa 36 ya Afrika ambao wanapanada mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuikumbusha jamii juu kupingana na vitendo vya unyanyasaji wa wananwake na wasichana.
Rais Kikwete akizungumza na wananchi waliofika wakati wa uzinduzi wa wapanda mlima Kilimanjaro,uzinduzi uliofanyika lango la kupandia mlima huo la Marangu

Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete akiwa amewasili mkoani Kilimanjaro apa alikuwa anasalimia na baadhi ya viongozi wa mkoa huo

Add caption

Wakuu wa wilaya za mkoa wa Kilimanjaro,toka shoto Anarose Nyamubi(Siha) Ibrahim Marwa(Same)Peter Toima(Rombo) na Athuman Mdoe (Mwanga) mwenye shati la kijani ni Katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro,Stephen Kazidi 
Mwenyeji wa ugeni huu ambaye ni mkuu wa mkoa wa |Kilimanjaro Leonidas Gama akiwa anawapa wageni wake histori fupi ya mkoa

                                            Viongozi mbalimbali wa mkoa wa Kilimanjaro.


Naibu Meya wa manispaa ya Moshi Vicent Limoyi(kulia) akiwa na baadhi ya viongozi wa wa vyama vya siasa na serikali.


                                                               Viongozi wa CCM.

Wazee wa mkoa wa Kilimanjaro.
Baadhi ya waandishi wa habari wakionekana kwambali wakifuatilia taarifa ya mkoa iliyokuwa ikitolewa na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro (hayupo pichani)

Mmoja wa wajumbe wa bodi mpya ya Kahawa walioteuliwa Bw Meynard Swai ambaye pia ni Meneja wa KNCU.Rais Jakaya Kikwete amemteua Bibi Eze Hawa Sumari kuwa mwenyekiti mpya wa bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kuchukua nafasi ya Pius Ngenze.

Ngeze amekuwa mwenyekiti wa bodi hiyo tangu mwaka 2008 hadi Desemba mwaka jana ambapo bodi yake ilimaliza muda wake wa uongozi

Tayari Ngeze na wajumbe wengine waliomaliza muda wao wameagwa rasmi na watumishi wa bodi hiyo katika hafla iliyofanyika February 27,2012

Sanjari na mwenyekiti huyo pia waziri wa kilimo,chakula na ushirika Prof Jumanne Maghembe ameteua wajumbe wapya watakaounda bodi hiyo.

Wajumbe hao ni pamoja na Fatuma Faraji ,Novatus Piigererwa, Yasinti Ngwasura na Eric Ng'maryo.

Wengine ni Maynard Swai ambaye ni Meneja wa KNCU,Prof James Terri ambaye ni mkurugenzi wa kituo cha utafiti wa zao la Kahawa(Tacri),Mh John Komba,mbunge wa jimbo la Mbinga na Eng Merad Omar Msuya.

at Tuesday, February 28, 2012 Posted by Daniel Mjema 0 Comments

Ndugu wafuatiliaji wa blog hii mpya ya taarifa za kichunguzi ,napenda kuwafahamisha kuwa mtandao huu wa kijamii bado uko katika hatua za mwisho za matengenezo ,tunajitahidi kuufanya ili uendane na hali halisi ya maisha na kisayansi zaidi ili kila mmoja aweze kupata huduma stahili.
Niwaombeni muendelee kuwa wavumilivu ,taarifa rasmi za uzinduzi wa blog hii tutawafahamisheni kupitia mitandano mingine na vyombo vingine vya habari.
KARIBUNI SANA.

Kundi la waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa changamoto ya kupanda mlima Kilimanjaro,Mlima mrefu kuliko yote barani Afrika.