MJEMA BLOG

JICHO LA MWANDISHI

  • RSS
  • Delicious
  • Digg
  • Facebook
  • Twitter

Siha .

MTOTO wa kike mwenye umri wa 18(jina tunalo) ambaye anatajwa kuwa mkazi wa Monduli Arusha na Dar es salaam, katika hali isiyo ya kawaida ameanguka katika kijiji cha Kishisha wilayani Siha kutokea angani jirani kabisa na mlima Kilimanjaro .


Tukio hilo la aina yake limetokea hivi karibuni majira ya saa 11 jioni wakati mtoto huyo akiwa na wenzake watatu wanaodaiwa kuwa wachawi walianguka muda mchache wakati wakijaribu kutua na Ungo waliokuwa wakiutumia kama usafiri  katika kijiji hicho kwa lengo la kutimiza malengo yao ya kishirikina.


Akizungumzia tukio hilo diwani wa kata ya Evaeni, Elinisaa Kileo
alisema mtoto huyo baada ya kuanguka na wenzake ambao hata hivyo walifanikiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha alijaribu kukimbilia katika msitu wa mlima Kilimanjaro ndipo wananchi wakafanikiwa kumkamta.


Alisema baada ya kukamatwa alipelekwa hadi katika eneo waliloangukia na kukuta vifaa vinavyosadikiwa kuvitumia katika shughuli zake za uchawi ambavyo ni vibuyu 8 vikiwa na Inzi ndani,Tunguli na dawa zingine ambazo hawakuweza kuzielewa pamoja na Ungo.


Kileo alisema baada ya kumkamata mtoto huyo walimfikisha kanisa la Kishisha kwa ajili ya maombi na baadae alipelekwa kituo cha polisi wilaya ya Siha kwa usalama zaidi kutokana umati wa watu uliofurika katika eneo hilo kumshuhudia mtoto huyo huku wengine wakishinikiza auawe.


“Kutokana na wingi wa watu waliokadiriwa kufikia 300 tulilazimika
kumpeleka kituoni hapo akiwa nusu uchi pamoja na vifaa vyake hivyo ambavyo hata hivyo wananchi walizuia visiingizwe kituoni kwa madai mapepo hayawezi ingia kituo cha polisi na badala yake wakashinikiza vichomwe moto”alisema Kileo.


Alisema kutokana na umati mkubwa kushinikiza kutolewa kwa vibuyu hivyo ndipo askari walilazimika kuwaruhusu pia kuondoka na binti huyo kutokana na kile kinachodaiwa kuwa serikali haiamini imani za kishirikina.


Diwani Kileo alisema mtoto huyo ambaye hakuweza kuzungumza
alirudishwa kwa mara nyingine kanisani ndipo akaanza kuzungumza kuwa alitumwa yeye na wenzake wakitokea  Dar es salaam  kwenda wilayani Siha kwa ajili ya kuroga na badala yake wakakosea njia wakiwa angani ndipo wakaanguka.


“Wakati tunamkamata binti huyo alikuwa Bubu ,baada ya maombi akaanza kufunguka,akasema yeye anatokea Dar es salaam ,mama yake ni mzaramo lakini baba yake ni wa wilaya ya Siha anaitwa Islael Masaki ambaye ni mwanajeshi na kwamba walitumwa kuja kuroga lakini wakakosea njia wakaanguka wenzake watatu wakatoroka.”alisema Kileo.


Alisema katika vifaa alivyokuwa navyo kilikuwepo kibuyu kikubwa
ambacho mototo huyo alisema kifaa hicho ndio gari kubwa kuliko yote ambalo limekuwa likitumiwa endapo wanasafiri wengi zaidi ya sabini na kwamba kimetumika kwa safari za bungeni wakati ule wa kumchagua spika.


“Alitueleza kuwa mara nyingi wamekuwa wakitumia hilo gari(kibuyu kikubwa) n aka maelezo yake amewahi kulitumia mpaka kule bungeni wakati ule wa kuchaguliwa spika wa bunge na amekuwa akilitumia kulingana na jinsi alivyotumwa na wakati mwingine amekuwa akienda nalo Nigeria hivi ndivyo alikuwa anatueleza”alisema Kileo.


Diwani Kileo alisema msichana huyo aliwaomba wasimfunge  kwa maelezo kuwa ataeleza wapi aliko Bibi yake aliyemtuma kufanya shughuli ,vifaa mbalimbali vinavyotumika pamoja namatukio waliyowahi yafanya wakati wakitekeleza maagizo ya Bibi huyo.


Hata hivyo binti huyo alifanikiwa kuwatoroka  na baadae baada ya
kumtafuta kwa muda mtrefu waligundua kuwa alionekana eneo la Samaki Maini kata ya Limishi ambako inadaiwa ni kwa shangazi yake huku taarifa zikisema tayari baba yake mzazi alifika kijijini hapo na tayari amempeleka Monduli anakoshi.


Tanzania daima lilimtafuta baba mzazi wa binti huyo  Islael Masaki
ambaye alikiri mwanaye huyo kuwa na matatizo na kwamba haelewi ana matatizo gani na ameacha shule muda mrefu kutokana na hali ya kupotea mara kwa mara na tayari amekwisha toa taarifa katika kituo cha polisi kadhaa.


“Mimi ni mzazi wake ,na ninachofahamu mimi mtoto wangu ana matatizo sielewi ana matatizo gani anaumwa muda mrefu ,na ameacha shule muda mrefu ,na huwa hakai nyumbani anaweza akaja nyumbani siku hiyo hiyo tena akapotea haonekani tena”alisema Masaki.


Alipoulizwa kuhusishwa kwa bibi yake katika kumtumia msichana huyo katika shughuli hizo za kishirikina Masaki alikanusha na kwamba mama yake(yaani bibi wa msichana) amekuwa mstari wa mbele katika kumshauri njia gani watumie katika kumsaidia msichana huyo.


“Hilo nakanusha ,nakanusha ,kwa maana ya kwamba sidhani kama mama yangu anaweza kuhusika katika suala hilo ,kwa sababu yeye mwenyewe amekuwa akinishauri juu ya huyo mtoto,ila mimi mtoto mwenyewe amewahi kunitajia mashangazi zake ndio wanafanya hivyo lakini bado sielewi ”alisema Masaki.


Masaki alisema mtoto huyo amekuwa akipotea na kurejea nyumbani hapo toka akiwa darasa la tano mwaka 2005 na kwamba hadi sasa hajafahamu nini afanye kwa bint huyo ili arejee katika hali ya kawaida kama aliyokuwa nayo awali.

Mwisho.

0 Responses so far.

Post a Comment