MJEMA BLOG

JICHO LA MWANDISHI

  • RSS
  • Delicious
  • Digg
  • Facebook
  • Twitter


Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Ngalawa akifungua mkutano wa siku ya wadau wa Mfumo wa Afya ya Jamii Mijini wa Tiba kwa Kadi (TIKA) ambapo Lengo la mkutano huo ilikuwa ni kuchukua maoni yao na kuwaeleza jinsi TIKA inavyofanya kazi. Kikao hicho kimefanyika leo Machi 28, 2014 katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe. Pembeni ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mheshimiwa Mrisho Gambo (kushoto) na Mwenyekiti wa Hamashauri ya Mji Korogwe ambaye ni Diwani wa Kata ya Kilole, Mheshimiwa Angello Bendera (kulia).
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mheshimiwa Mrisho Gambo akitoa ufafanuzi wa jambo mbele ya mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Ngalawa (kushoto). Pembeni ni Diwani wa Kata ya Mgombezi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya, Maji na Uchumi, Mheshimiwa Omari Chafesi na Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) – Mkoa wa Tanga, Bw. Ally Mwakababu (kushoto).
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) – Mkoa wa Tanga, Bw. Ally Mwakababu akieleza umuhimu wa matumizi ya Tiba kwa Kadi (TIKA) mbele ya mkuu wa mkoa wa Tanga.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe ambaye ni Diwani wa Kata ya Kilole, Mheshimiwa Angello Bendera (kushoto) akiendesha mkutano wa siku ya wadau wa Mfumo wa Afya ya Jamii Mijini wa Tiba kwa Kadi (TIKA) ambapo Lengo la mkutano huo ilikuwa ni kuchukua maoni yao na kuwaeleza jinsi TIKA inavyofanya kazi. Pembeni ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Bw. Lewis Kalinjuna na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya mji Korogwe, Dokta Jerry Mwakanyamale.
Afisa Matekelezo na Uratibu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) – Singida, Bw. Issaya Shekifu akitoa uzoefu wake katika moja ya Wilaya ya Ilamba, Singida jinsi wananchi wanavyofaidika na TIKA.
Viongozi wa Dini wakifuatilia mkutano wa siku ya wadau wa Mfumo wa Afya ya Jamii Mijini wa Tiba kwa Kadi (TIKA) ambapo Lengo la mkutano huo ilikuwa ni kuchukua maoni yao na kuwaeleza jinsi TIKA inavyofanya kazi.
Wananchi wa Mji wa Korogwe wakifuatilia mkutano wa siku ya wadau wa Mfumo wa Afya ya Jamii Mijini wa Tiba kwa Kadi (TIKA) ambapo Lengo la mkutano huo ilikuwa ni kuchukua maoni yao na kuwaeleza jinsi TIKA inavyofanya kazi.
Wananchi wa Mji wa Korogwe wakifuatilia mkutano wa siku ya wadau wa Mfumo wa Afya ya Jamii Mijini wa Tiba kwa Kadi (TIKA) ambapo Lengo la mkutano huo ilikuwa ni kuchukua maoni yao na kuwaeleza jinsi TIKA inavyofanya kazi.
Wananchi wa Mji wa Korogwe wakifuatilia mkutano wa siku ya wadau wa Mfumo wa Afya ya Jamii Mijini wa Tiba kwa Kadi (TIKA) ambapo Lengo la mkutano huo ilikuwa ni kuchukua maoni yao na kuwaeleza jinsi TIKA inavyofanya kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Ngalawa akisalimiana na Mjumbe wa Kamati ya Msikiti Mkuu Manundu, Korogwe Mzee Daffa Daffa.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Ngalawa akisalimia na viongozi wa dini wa Halmashauri ya Mji Korogwe mara baada ya kumaliza kufungua mkutano wa siku ya wadau wa Mfumo wa Afya ya Jamii Mijini wa Tiba kwa Kadi (TIKA) ambapo Lengo la mkutano huo ilikuwa ni kuchukua maoni yao na kuwaeleza jinsi TIKA inavyofanya kazi.
Waheshimiwa Madiwani wa Kata mbalimbali za Halmshauri ya Mji Korogwe wakiwa katika mkutano wa siku ya wadau wa Mfumo wa Afya ya Jamii Mijini wa Tiba kwa Kadi (TIKA) ambapo Lengo la mkutano huo ilikuwa ni kuchukua maoni yao na kuwaeleza jinsi TIKA inavyofanya kazi.
NHIF 11: Afisa Matekelezo na Uratibu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)- Dar es Salaam, Genoveva Vicent akitoa majumuisho jinsi Mfumo wa Afya ya Jamii Mijini wa Tiba kwa Kadi (TIKA) unavyoweza kuwasaidia wananchi.


 Mchungaji Joseph Mhina wa Kanisa la Anglikana Manundu, Korogwe akitoa shukrani kwa wananchi waliofika katika mkutano huo wa wadau. 
Timu ya Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dar es Salaam na Tanga waliokuwa wakiratibu mkutano huo wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa na Wilaya. Picha zote na Cathbert Kajuna wa Kajunason Blog.

at Saturday, March 29, 2014 Posted by Daniel Mjema 0 Comments

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda Leo atakuwa mgeni rasmi katika hafla ya kukabidhi Tuzo ya Mwanamke Bora wa Mwaka 2013-14, itakayowakutanisha wanawake wanne itakayofanyika kesho katika Ukumbi wa The African Dream mjini Dodoma.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ndiye atakuwa mgeni rasmi katika utoaji tuzo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers, ambayo ndiyo iliyoratibu zoezi hilo, Eric Shigongo, alisema jana kwamba shughuli hiyo itakuwa ni hitimisho la kazi kubwa ya kupokea na kuchuja kura zilizotumwa na wasomaji kumtafuta mwanamke bora ambaye ni nembo kwa taifa.
Prof. Anna Tibaijuka.
“Zoezi hili lilifanyika kwa muda wa miezi tisa, kuanzia Juni mwaka jana hadi Machi mwaka huu. Awali kabisa watu walitakiwa kutuma majina ya wanawake wanaowaona ni bora ili wapigiwe kura, watu waliitikia vizuri sana, kwani jumla ya majina 150 yalitumwa katika kipindi cha miezi miwili.
Dk. Asha Rose Migiro.
“Baada ya hapo majina hayo yakaandikwa katika magazeti na watu wakatakiwa kupiga kura ili kuwatoa wanawake ambao wanadhani hawakustahili tuzo hizo,” alisema Shigongo, ambaye kampuni yake inatoa magazeti ya Uwazi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Amani, Risasi na Championi.
Alisema katika awamu ya kwanza ya miezi hiyo miwili, majina ya wanawake 20 yaling’ara na hivyo kuingia katika awamu nyingine ya kupigiwa kura, ambapo baada ya muda kama huo pia, wanawake kumi walipata alama nyingi na hivyo kuingia katika awamu ya tatu na ya mwisho.
Mh. Anne Kilango Malechela.
Alisema kwenye hatua hiyo ya mwisho, wanawake watano walipita ambao ni Ananilea Nkya, Anna Tibaijuka, Anna Kilango Malecela, Asha Rose Migiro na mama Maria Kham. Katika zoezi hilo, wanawake hao wenye mvuto katika jamii walichuana na mmoja wao, Nkya, kuondolewa baada ya kura zake kutotosha kwa ajili ya fainali,” alisema Shigongo.
Dk. Maria Kamm.
Kwa upande wake, mratibu wa Tuzo hizo, Luqman Maloto, alisema tukio hilo la kihistoria ambalo pia litashuhudiwa na wabunge wa Bunge la Katiba walio mjini Dodoma, litaambatana na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali, akiwemo Linah,” alisema Maloto.

at Saturday, March 29, 2014 Posted by Daniel Mjema 0 Comments
at Saturday, March 29, 2014 Posted by Daniel Mjema 0 Comments

Na Mwandishi wetu,  Aliyekuwa Handeni
 
WANANCHI wa Kijiji cha Komsala, wilayani Handeni, mkoani Tanga, wamemlalamikia mwekezaji anayejulikana kwa jina la Amina Singa, kuwa anapora ardhi zao, huku serikali ya Kata Kwamatuku, ikishindwa kuwatetea wakulima wadogo na kuelemea upande wa mwekezaji.
Katibu wa Baraza la Kata ya Kwamatuku, Nassib Bakari, pichani.
 
Mwandishi wa habari hizi alitembelea katika kijiji hicho na kufanya mazungumzo na wananchi sambamba na Baraza la Kata juu ya mgogoro huo unaosababisha malalamiko mengi kutoka kwa wakulima hao.
Mjumbe wa Baraza la Kata ya Kwamatuku, Mwanahamisi Nyata, pichani.
Akizungumza kwa huzuni kubwa, mkulima aliyejitambulisha kwa jina la Hausi Zuberi, alisema kuwa mwekezaji huyo amechota eneo lake, kama alivyofanya hivyo kwa wananchi wengine waliopakana na shamba lake.
 Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu pichani.
Alisema hali hiyo imewafanya waishi kwa mashaka wakiamini kuwa ataendelea na tabia yake hiyo, licha ya kumiliki eneo zaidi ya heka 120 hali ya kuwa anashindwa kulilima.
Hausi Zuberi, mmoja wa walalamikaji wa migogoro ya ardhi katika Kata ya Kwamatuku, wilayani Handeni, mkoani Tanga.
“Mwekezaji huyu ni kero kubwa kwetu kwasababu amechota maeneo yetu wakulima tusiopungua 6 baada ya kuvuka mbele ya mpaka wake, hali inayotufanya tuishi kwa hofu tukiamini kuwa ataendelea kutupora,” alisema.

Naye Paulina Athon Simbaulanga, alisema kuwa uporaji huo umebarikiwa na Baraza la Kata, baada ya kutembelea eneo hilo, jambo linalowafanya waamini kuwa kuna njia ya mkato iliyopitwa katika kufanikisha uporaji huo.

“Amina alikuja kijijini kwetu na kuomba heka 60, lakini sasa ana heka 120 na bado anapora sisi tusiokuwa na hata heka 5, licha ya yeye kumiliki eneo kubwa.

“Hatujui hizo heka nyingine amezipata vipi na sheria za ardhi zinasemaje katika hilo, ingawa serikali ya kijiji inajua na mgogoro huu umebarikiwa na viongozi wetu,” alisema.

Alipotafutwa Amina, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwakuwa wananchi hao ndio waliovamia shamba lake, licha ya kushindwa kusema ni kiasi gani cha shamba analomiliki kijijini hapo kutoka heka 50 zinazotakiwa kisheria.

“Kwanza mtakuwa umefanya makosa kama mmeamua kufanya mazungumzo na wananchi hao kabla yangu, hivyo siwezi kusema lolote,” alisema Amina.

Katibu wa Baraza la Kata ya Kwamatuku, wilayani Handeni, mkoani Tanga, Nassibu Bakari Bigo, alikiri kuupokea mgogoro huo wa Amina na wakulima wa kijiji cha Komsala, huku akisema kesi za aina hiyo zimeendelea kushamiri katika maeneo mengi katika Kata hiyo.

“Tuliupokea mgogoro huo, lakini kwa kiasi kikubwa umechangiwa na serikali ya kijiji husika kwa kushindwa kutatua kesi hizo na watu kusaka haki yao Baraza la Kata,” alisema Bakari.

Kwa mujibu wa Bakari, kesi za migogoro ya ardhi zimeshamiri katika eneo lao, hivyo viongozi wa vijiji wanapaswa kusimamia vyema sheria za ardhi, huku wakitoa elimu kwa wakulima na wananchi wao, wakiwamo walalamikaji wa kesi inayomhusisha Amina, kutokana na mashahidi wao kushindwa kufika walipoitwa na Baraza la Kata.

at Saturday, March 29, 2014 Posted by Daniel Mjema 0 Comments


.Asema mgombea Urais anamwandama. Akaunti Feki ya Facebook yamtesa

MBUNGE WA MOSHI VIJIJINI-DKT. CYRIL CHAMI

Ripota Wetu, Moshi 

Jinamizi la Urais linazidi kutikisa medani za siasa nchini, baada ya Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Dk. Cyril Chami (CCM) kudai anaandamwa na mtandao wenye malengo ya Urais 2015.
 
Dk. Chami amedai kiini ni mbabe mmoja ambaye hakumtaja, mwenye uwezo wa fedha kukasirishwa naye, baada ya kukataa maagizo yake kwamba amsaidie swahiba wake anayewania Urais mwaka 2015.
“Niliikataa kazi hiyo kwa sababu haina maslahi kwa Taifa wala Moshi Vijijini…Mimi nitamuunga mkono mgombea Urais yeyote atakayechaguliwa na mkutano mkuu wa CCM,”alisema Dk. Chami.
Dk. Chami aliongeza kusema,”Haitanishangaza ikithibitishwa kuwa mbabe huyu ndiye anatoa fedha kuufadhili mtandao huu wa wahalifu, japo hii ni kazi ya Polisi na ni kazi inayoendelea,”
Mbunge huyo amedai mtandao huo, ndio ambao umefungua  akaunti yenye jina lake na picha katika mtandao mashuhuri wa kijamii wa Facebook na kumchonganisha na wapiga kura wake na CCM.
Katika taarifa yake kwa gazeti hili jana, Dk. Chami amedai akaunti hiyo inatumika kumchonganisha na chama chake pamoja na viongozi wakuu wa CCM ili asiteuliwe kugombea ubunge mwaka 2015.
“Kwa kujifanya wao ni mimi, wanapingana na misimamo yote ya CCM. Kwa mfano, wanadai kuwa kwenye mchakato unaoendelea wa Bunge la Katiba, mimi napendelea serikali tatu,”amelalamika.
Akitoa mfano wa hivi karibuni kabisa, Dk. Chami amedai Jumapili iliyopita, watu hao walitoa taarifa kuwa ana mashaka CCM itashindwa huko Kalenga kwa kuwa mara zote kinashinwa chaguzi ndogo.
 “Eti mimi napendelea kura ya siri katika Bunge la Katiba linaloendelea…. Naonyeshwa kuwa mtetezi wa CHADEMA na kutabiri ushindi wa Chadema huko Kalenga na Chalinze”amelalamika Dk. Chami.
Dk. Chami amesema akaunti hiyo ya Facebook sio yake na kwamba kama analo jambo anataka kuzungumza na wapiga kura wake, atawafuata jimboni na si kuzungumza nao kupitia Facebook.
Pia amesema tayari amewasiliana na viongozi wa CCM juu ya uwepo wa uhalifu huo ambao lengo ni kutaka kumuonyesha kuwa yeye ni msaliti ndani ya CCM jambo ambalo hata halifikirii kulifanya.
Dk. Chami amekilaumu kitengo kinachoshughulikia makosa ya mitandaoni (Cyber Crime Unit) kwa kushindwa kuifunga akaunti hiyo na kuwakamata walioifunga na wanaoendelea kuitumia.
“Tena akaniambia waliomba msaada TCRA (Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania) ili akaunti hii ifungwe, nao TCRA wameshindwa”alilalamika Dk. Chami.
“Hadi leo akaunti inatumika naendelea kutengenezewa maadui ndani ya CCM na kwa viongozi wa juu wa nchi na wahalifu hawa wako huru wakiendelea kuchekelea maumivu wanayonisababishia”amedai.
Dk. Chami amesema japo ameshauri na Polisi kwamba naye aingie Facebook na kuwajibu wahalifu hao, kamwe hatafanya hivyo kwani anaweza kuchochea taarifa mbaya zaidi kuliko sasa.
“Nimekataa kwa sababu kama wahalifu wameweza kuniundia akaunti na Dola imeshindwa kunilinda, nikiunda akaunti yangu wataiingilia na hiyo na wataandika mabaya kuliko wanayoyaandika”alisema.
Dk. Chami alisema kama wahalifu hao wataweza kuingilia akaunti yake na kuandika mabaya zaidi kwenye akaunti yake halali, watasherehekea na kuhalalisha uovu wao huo.
Soma taarifa yake kamili hapa chini
Naitwa Dr Cyril August Chami,  Mbunge wa Moshi Vijijini Mkoa wa Kilimanjaro,  Tanzania.  Kwa miezi kadhaa sasa kuna mtu au kikundi cha watu ambaye/ambacho kimeunda akaunti feki kwenye Facebook kwa jina langu na kuitumia akaunti hiyo.

kunichonganisha na Chama cha Mapinduzi (CCM) na viongozi mbali mbali nchini Tanzania kwa lengo kuu moja: kunipaka matope na kuichafua taswira yangu mbele ya umma na ndani ya CCM. 

Wanachokilenga (na hapa natumia wingi kwa sababu ndivyo nimeelezwa na Cyber Crime Unit of the Police Force Tanzania) ni kupambana nami kupitia mitandao ili tu 2015 nisiteuliwe na CCM kuendelea kugombea ubunge Jimbo la Moshi Vijijini,  ateuliwe mwanachama mwingine wanayemtaka wao!
Kwa kujifanya wao ni mimi, wanapingana na misimamo yote ya CCM. Kwa mfano, wanadai kuwa kwenye mchakato unaoendelea wa Bunge la Katiba, mimi napendelea serikali tatu. Eti mimi napendelea kura ya siri katika Bunge la Katiba linaloendelea.

 Naonyeshwa kuwa mtetezi wa CHADEMA.  Hata katika uchaguzi uliofanyika March 16 Kalenga eti naonyeshwa "kutabiri" ushindi wa CHADEMA na pia eti "nimetabiri" ushindi wa CHADEMA Chalinze! 

Naonyeshwa nikijinasibu kuwa eti Chama changu CCM huwa kinashindwa chaguzi ndogo, kwa hiyo na hizi mbili CCM ijiandae kushindwa! Wahalifu hawa wanayatuma maoni haya yote kwa niaba yangu huku wakisahau kabisa kuwa ni hivi majuzi tu tarehe 9 Februari CCM ilivigalagaza vyama vya upinzani kwenye uchaguzi MDOGO wa madiwani kwa kushinda katika kata 23 kati ya kata 27. 

Ama kwa makusudi kabisa, ama kwa upungufu wao wenyewe wa kumbukumbu, au kwa ushabiki wao kwa upinzani, wanatabiri kwa  niaba yangu kuwa CCM ni dhaifu kwenye chaguzi ndogo, kitu ambacho ni kichekesho kwa sababu takwimu ziko wazi: 

CCM imewika uchaguzi mdogo wa madiwani, CCM imewika Kalenga, na kila mtu anayefahamu siasa angalau ya darasa la saba anajua kuwa CCM itawika Chalinze!

Kutokana na uhalifu huu, nimechukua hatua zifuatazo:
Kwanza nimeikana akaunti hiyo ya Facebook. Siyo yangu na situmii mitandao ya kijamii katika siasa kwa sababu kuu mbili. 

Sababu ya kwanza ni kwamba asilimia kubwa ya walioniajiri yaani wapigakura wa Moshi Vijijini hawatumii mitandao ya jamii. Kwa hiyo hata kama ningeandika mafanikio yote ya uongozi wangu kwenye Facebook ni asilimia ndogo sana ya wapiga kura wangu ingenisoma. Ni kweli kuwa Watanzania wanaoishi mijini au kwenye diaspora wangeelewa, lakini mwisho wa yote wengi wao hawatapanda ndege au magari ili tu kwenda Moshi Vijijini kunipigia kura.  

Nitoe mfano kuwa mwaka 2005 ilipigwa kura ya maoni kwenye mtandao mmoja wa jamii kuhusu nani angeshinda ubunge Moshi Vijijini. Mgombea wa CHADEMA "alishinda" kwa asilimia 80. Mimi "niliambulia" asilimia 20. Kwenye uchaguzi "halisi" nilipata kura 49,000 na mgombea wa CHADEMA akapata kura 18,000!
Pili, badala ya kuandika kwenye Facebook au mitandao mingine ya kijamii, nimegundua njia rahisi na yenye uhakika ya kuwaongoza wananchi walionichagua. Njia hiyo ni kuwafuata huko waliko. 

Katika miaka takriban tisa ya ubunge wangu nimewatembelea wapiga kura wangu walio katika vitongoji 322, vijiji 67 na kata 16 kuliko mbunge mwingine yeyote tangu Tanzania iwe huru. Kwa hakika, takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya ziara zangu za miaka tisa inaizidi jumla ya ziara za watangulizi wangu wote kwa miaka 40. 
Hii haina maana kuwa sikutani na wapiga kura wangu wanaoishi nje ya jimbo. La hasha! Bado nakutana nao. Kwa mfano, tarehe 2 Februari mwaka huu nilikutana na wapiga kura wangu wanaotoka Kata ya Uru Mashariki (Kinyamvuo) waishio Dar es Salaam ukumbi wa Chuo cha Maji.

 Baada ya kuwaeleza hali ya kata yao na kuyajibu maswali yao, msemaji aliyesimama kunishukuru, Mheshimiwa DC mstaafu Clemence Orauya, alikiri kuwa katika hadhira ile ya watu karibu 300 hakuweko mtu anayeifahamu jiografia ya kata ile kama mimi, japokuwa mimi si mzaliwa wa kata hiyo. Aliungwa mkono na karibu kila aliyehudhuria. 
Kwa ufupi, Facebook haiwezi kumfikia mwananchi aliyeko kitongoji cha Uhondo au Saningo au Mandaleni au Msarikie ambako kote hakuna umeme achilia mbali mtandao; mbunge anaweza. Facebook haiwezi kusimamia ujenzi wa barabara za Kibosho na Uru kwa kiwango cha lami; mbunge anaweza.

Facebook haiwezi kuikumbusha Serikali  ianzishe ujenzi wa barabara ya lami ya Old Moshi kama ilivyoahidiwa; mbunge anaweza. Facebook haiwezi kusimamia sekta ya elimu Moshi Vijijini;  mbunge anaweza. Facebook haitatatua tatizo la maji katika Skimu ya Umwagiliaji Lower Moshi; mbunge anatatua kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali.
Hatua ya pili niliyochukua ni kuwasiliana na uongozi wa CCM ngazi za wilaya, mkoa na taifa kuwaeleza juu ya uwepo wa uhalifu huu. Hivyo, picha inayotengenezwa kuwa mimi ni msaliti ndani ya CCM ni sawa na kumtupia tope mtu aliyejipaka mafuta! Tope zote zinadondoka bila kumchafua mlengwa.
Hatua ya tatu ni kutoa taarifa Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam Kitengo cha Makosa ya Uhalifu kwenye Mitandao (Cyber Crime Unit) ili wanisaidie kuifunga hiyo akaunti na kuwakamata wahalifu. Kwa masikitiko makubwa sana wameshindwa yote mawili. Hadi leo akaunti inatumika; hadi leo naendelea kutengenezewa maadui ndani ya CCM na kwa viongozi wa juu wa nchi; na hadi leo wahalifu hawa wako huru wakiendelea kuchekelea maumivu haya wanayonisababishia. 

Nina hakika watakaposoma ujumbe huu watakuwa hawana mbavu kwa vicheko huku wakijipongeza kwa kuyafanikisha malengo yao.
Kwa masikitiko makubwa zaidi, kiongozi wa Cyber Crime Unit ameniambia wameshindwa yote mawili!!!! Wameshindwa kuifunga akaunti hiyo;

na wameshindwa kuwatambua wahalifu hao, na kwa maana hiyo wameshindwa kuwakamata. Walichofanikiwa hadi sasa ni jambo moja tu, nalo ni kugundua kuwa uhalifu huu unafanywa na kikundi cha watu waliojipanga kiujanja kiasi kwamba wao (Cyber Crime Unit) wamewashindwa. Tena akaniambia waliomba msaada Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (Tanzania Communications Regulatory Authority-TCRA) ili akaunti hii ifungwe, nao TCRA wameshindwa!
Nayaandika haya yote kwa sababu mbili. Sababu ya kwanza ni ile inayotegemewa na msomaji yeyote, nayo ni ile ya haki yangu binafsi. Naamini ninayo haki ya kulindwa kutokana na uhalifu huu kama msomaji yeyote alivyo na haki hiyo. Binafsi natambua wahalifu hawa wanachokilenga ni kimoja tu: Dr Chami asiwe tena mbunge wa Moshi Vijijini kuanzia 2015.

 Wanajua hadi sasa hakuna mwana CCM mwenye ubavu wa kunishinda katika kura ya maoni mwakani. Hivyo njia pekee ni kunichonganisha na wakuu wangu wa CCM ili nitakaposhinda kura ya maoni, ngazi za juu za CCM ziache kuniteua ateuliwe mtu mwingine. Kwao haijalishi kama mgombea huyu mbadala atakipatia ushindi CCM.

 Kwao ni heri upinzani uchukue jimbo lile kuliko Dr Chami awe mbunge. Kwa ufupi, hawa sio wapenzi wa CHADEMA au CCM. Ni wababe wenye fedha wanaoamini wana uwezo wa kumuinua yeyote awe mbunge na kumshusha yeyote asiwe mbunge.

 Na kwa sababu walishanieleza nia yao hiyo na nimeyaeleza haya yote kwa Polisi, najisikia huru kuwaeleza wasomaji kiini cha tatizo lenyewe. Kiini ni kwamba mbabe mmoja mwenye fedha amekasirishwa nami kwa sababu nimekataa maagizo yake kuwa nimsaidie swahiba wake anayewania Urais 2015! 

Niliikataa kazi hiyo kwa sababu moja tu: Haina maslahi kwa Taifa wala Moshi Vijijini!!!!! Mimi nitamuunga mkono mgombea Urais yeyote atakayechaguliwa kwenye mkutano mkuu wa CCM, siye mgombea ninayelazimishwa nimuunge mkono nje ya mfumo halisi wa CCM na kinyume na dhamira yangu.
 
Haitanishangaza ikithibitishwa kuwa mbabe huyu ndiye anatoa fedha kuufadhili mtandao huu wa wahalifu, japo hii ni kazi ya Polisi na ni kazi inayoendelea. Kama mtandao huu utashinda au utashindwa ni jambo la "tusubiri tuone". 

Ninalothibitisha kwa wasomaji ni kuwa mimi nitaendelea kuwa mwaminifu kwa wapigakura wangu wa Moshi Vijijini na kwa Chama cha Mapinduzi (CCM). Wao wakiamua niendelee kuwawakilisha nitaendelea.  Wakinitaka nipumzike nitayaheshimu maamuzi hayo na nitafanya mambo mengine. Ikumbukwe kuwa kabla ya kuwa mbunge sikuwa barabarani.  Nilikuwa nafanya kazi na nitaendelea kufanya kazi.
 
Sababu ya pili iliyonifanya niandike ujumbe huu ni kuonyesha hofu yangu kwa nchi yetu ya Tanzania  kuwa uhalifu unaweza kufanywa NA VYOMBO HUSIKA VYA DOLA VIKAKIRI KUSHINDWA. The Cyber Crime Unit of the Police Force and the TCRA have both confirmed their helplessness on this matter! 
Hii ina maana gani?
Ina maana kuwa wakimalizana nami watafanya hivyo kwa yeyote wanayemchukia na vyombo vya dola vitakiri kuwa haviwawezi. Lakini mbaya zaidi, wataiingilia sekta ya fedha na kuwaibia wananchi bila huruma na vyombo vya dola vitakiri kuwa hawawawezi wahalifu hawa!
 
Nimeshauriwa na Cyber Crime Unit kuwa nami niingie Facebook kuwajibu wahalifu hawa. Nimekataa kwa sababu kama wahalifu wameweza kuniundia akaunti na dola imeshindwa kunilinda, nikiunda akaunti yangu wataiingilia na hiyo na wataandika mabaya kuliko wanayoyaandika kwenye akaunti waliyounda wao. 

 Hii ni kwa sababu kwenye akaunti waliyounda wanaogopa kufanya uharibifu mkubwa wakijua kuwa siku si nyingi watagunduliwa. Lakini wakiweza kuiingilia akaunti niliyoisajili mwenyewe watasherehekea kwa sababu wataweza kuandika mabaya zaidi kupitia akaunti yangu halali na kuyahalalisha kabisa haya ambayo wameshaandika. 

 Hapo hata wale wasomaji wanaoamini kuwa nahujumiwa wataniona msanii na CCM wataniita rasmi msaliti. Lengo la wahalifu litatimia na Cyber Crime Unit wataendelea kuniambia wameshindwa kuwapata "perpetrators" hao.
Wasalaam,
Dr Cyril Chami.

at Saturday, March 29, 2014 Posted by Daniel Mjema 0 Comments

Ripota Wetu,  Same

WATU 12 wamefariki dunia na wengine 7 kujeruhiwa kwenye ajali mbaya iliyotokea jana, majira ya saa mbili usiku katika eneo la Hedaru, kata ya Hedaru, Tarafa ya Chome Suji, wilaya ya Same, barabara kuu ya Tanga/Moshi.

Ajali hiyo kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Mkuu wa wilaya ya Same, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo, Herman Kapufi ilitokea baada ya gari lenye namba za usajili T.299 ANM aina ya Fuso lori, ambalo lilikuwa likitokea Moshi kuelekea Dar es salaam kugonga gari lenye namba za usajili T.170 AKZ Toyota Hilux kwa nyuma.

Kapufi alisema gari hiyo aina ya Toyota iliyokuwa ikiendeshwa na Diwani wa kata ya Hedaru, Gerard Mgwena, ikitokea Hedaru kuelekea Majengo, likiwa limebeba waombolezaji waliokuwa wanakwenda kwenye msiba wa mtoto ambaye jina lake halikufahamika mara moja, aliyefariki dunia baada ya kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha Hedaru.

“Gari lililokuwa limebeba waombolezaji wanawake wapatao 20, walikuwa wanaenda kwenye msiba wa mtoto aliyesombwa na maji, walipofika katika eneo la Mnara wa simu, kwenye daraja, Yule dereva wa Hilux akaona maji mengi akataka kuyavuka kumbe lilikuwa ni Tope, akakwama, muda mfupi likaja gari aina ya fuso na kumgonga kwa nyuma,” alisema.

Alisema baada ya kugongwa kwa nyuma, lile Hilux iliyokuwa ikiendeshwa na Diwani huyo, iligonga gari yenye namba za usajili, T.737 AKW kabla ya kugonga tela namba za usajili T.776 CCN scania lori, likiendeshwa na Gabriel Daudi (35), mkazi wa Moshi, likitokea Dar es salaam kueleka Moshi.

“Baada ya kugongwa kwa nyuma gari lile liligonga magari mengine kwa nyuma, watu 10 waliokuwa  katika ile Hilux walifariki palepale na wengine 10 wakajeruhi ila leo asubuhi tumepata habari kuwa wamefariki wengine 2 na kufanya idadi kufikia 12,” alisema Kapufi.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, ACP- Robert Boaz, aliwataja Marehemu kuwa ni Stella John (45), Salma Kizoka (33), Merry Senzige (49), Neema Daniel (52), Rehema George (29), Sofia Mbike (51), Mamaritha Kalani (55) na Mamakalani Stephano.

Wengine ni Kolina Masi (55), Bahati Daudi (25), Farida Kyondo (24) na Maria John (33) wote ni wakulima na wakazi wa Kongei Hedaru na kwamba katika ajali hiyo pia kulikuwa na majeruhi 7, watatu kati yao wakiwa na hali mbaya.

Kamanda Boaz aliwataja majeruhi hao kuwa ni Zubeda Mrindoko (42), Nipa Chedieli (29), Zubeda Mlitha (32) ambao wana hali mbaya na wamelazwa katika Hospitali ya rufaa KCMC huku wengie wenye hali nzuri wakiwa ni na wengine wenye Joyce Kondogwe (29), Subira Juma (22), Ramadhani Msangi (31), Dereva na Adinani Rajabu (31), ambaye ni Dereva, na kwamba miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Same.

Kamanda Boaz alisema jeshi la polisi mkoani hapo linawasaka madereva wawili wa Toyota Hilux ambaye ni Diwani wa kata ya Hedaru na Dereva wa Fuso ili hatua za kinidhamu ziwezekuchukua mkondo wake huku akibainishwa kuwa chanzo cha ajali hiyo kuwa ni utelezi wa udongo uliokuwa umejaa barabarani kutokana na mvua kubwa iliyosomba maji na udongo kutoka maeneo ya milimani.

“Dereva wa gari la Toyota hilux, alipofika eneo hilo gari ilizima ghafla kutokana na udongo mwingi uliojaa barabarani pamoja na uitelezi, na gari aina ya fuso ilipojaribu kusimama ilishindwa kutokana na utelezi na kuigonga hilux kwa nyuma ndipo gari zote zikaingia barabarani upande wa kulia na kugongana na gari lingine aina ya fuso,” alisema Boaz.