MJEMA BLOG

JICHO LA MWANDISHI

  • RSS
  • Delicious
  • Digg
  • Facebook
  • Twitter

Regina Kihosa (62), mkazi wa Kosolameba mkoani Kigoma amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kufuatia gonjwa la ajabu lililompata huku akidai kwamba limetokana na wachawi ambao wanausumbua mji wake.

Regina Kihosa akiteseka kwa gonjwa la ajabu.

KWANZA AMEPOTEZA WATOTO WANANE
Mama huyo amelazwa katika hospitali hiyo jengo la Sewahaji,wodi namba 24 akiendelea na matibabu na ana mawazo mengi kwa kile anachokidai kwamba wachawi wanachezea mji wake na kati ya watoto wake kumi aliowazaa wanane wamefariki kwa muda mfupi kwa magonjwa ambayo wakipimwa hospitalini hayaonekani.

Aliendelea kudai kwamba watoto wake wawili waliobaki wamekua waoga na  wamekimbia kutoka nyumbani kwake kuhofia kurogwa na kuuawa pia mume wake aliyemtaja kwa jina la Ndeki Mashati naye alifariki kwa gonjwa la ajabu la kujaa maji tumboni.
Regina akizungumza kwa shida huku akionekana mwenye uso wa majonzi na mawazo mengi alikuwa na haya ya kusema:
“Gonjwa linalonitesa lilianza mwaka jana kwa kuumwa chini ya meno huku maji yakitoka sehemu hiyo, baadaye ulitokea uvimbe chini ya ulimi ambao kadiri siku zilivyokwenda uliongezeka kukua ndipo nilipelekwa Hospitali ya Mkoa Maweni kule Kigoma lakini sikuweza kupata tiba na kurudi nyumbani kutokana na ugonjwa kutojulikana.
Regina Kihosa akiwa hospitali ya Taifa Muhimbili akisumbuliwa na ugonjwa usiojulikana.

“Hali yangu nikiwa nyumbani ilizidi kuwa mbaya, sikuwa na mtu wa kunihudumua wala kuniliwaza, ingawa madaktari wa Maweni walinishauri nije Muhimbili lakini kutokana na umaskini nilikata tamaa, sikuwa na nauli, nilitamani Mungu achukue uhai wangu kuliko kupata maumivu makali kiasi hiki, nashindwa kula nashindia uji.
KUCHANGIWA NAULI
“Watoto wangu wawili waliobaki walikuwa na hofu wakawa wanatangatanga baada ya kuwaona ndugu zao wanane walivyokufa vifo vya kutatanisha kwa muda mfupi wa miaka minne, walikimbia, nilibaki nyumbani peke yangu, nilifikiri jinsi ya kufika Muhimbili bila mafanikio, namshukuru Mungu alinipa nguvu ya kwenda kanisani kutoa kilio changu na mikachangiwa shilingi elfu sitini.

“Baada ya kupata fedha hizo nilijikongoja hadi kituo cha mabasi nilipata usafiri hadi Tabora, nililala pale katika kituo cha mabasi kesho yake nilikuja hapa Dar nilifika Kituo cha Mabasi Ubungo usiku saa sita, nililazimika kulala kituoni kwani sikuwahi kufika wala sina ndugu hapa jijini, kesho yake nilipanda daladala hadi Muhimbili.
“Ninawashukuru waumini wa kanisa walionichangia kwani baadhi ya wananchi walisema wamechoka kunichangi kutokana na misiba ya kila kukicha, nilijisikia vibaya kwani mimi sikupenda wanangu wafe ili nipate michango yao.
AOGOPA KURUDI KWAKE
“Nawahukuru sana madaktari wa hapa Muhimbili kwani tangu nije mwishoni mwa mwezi wa tatu wamekata nyama ya mdomoni na kuifanyia uchunguzi pia wamechukua vipimo vingine ikiwa ni pamoja na kunipiga picha ya x ray.

Na kuhusu  chakula wananijali sana, kinachoniumiza ni kwamba hata nikipona nitaenda wapi? Pale kwangu hakuna amani tena, napaogopa,  nikiangalia makaburi ya watoto wangu na mume wangu nashindwa kulala,” alisema mama huyo huku akitokwa machozi
Mama huyo anaomba msaada kwa wasamaria wema kumsaidia, aliyeguswa awasiliane na afisa ustawi ya jamii wa Muhimbili ambaye yupo naye karibu kwani yeye hana simu. Anapatikana kwa namba  0683 406680.

0 Responses so far.

Post a Comment