MJEMA BLOG

JICHO LA MWANDISHI

  • RSS
  • Delicious
  • Digg
  • Facebook
  • Twitter

.Adaiwa kumpa kazi hiyo Shariff
.Adaiwa kupokea mrejesho baada ya mauajiMfanyabiashara tajiri wa Mererani, Joseph Mwakipesile “Chusa”, amedaiwa ndiye aliyetoa maelekezo ya kuuawa kwa mfanyabiashara mwingine tajiri wa Mererani, Erasto Msuya.Chusa alikuwa ni mmoja wa washitakiwa wa kesi hiyo ya mauaji ya kukusudia, kabla ya Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), kumuondoa katika kesi hiyo Aprili 16 mwaka huu.DPP alitumia mamlaka aliyopewa kisheria chini ya kifungu namba 91 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002, kumfutia mfanyabiashara huyo shitaka hilo.Kifungu hicho kinatamka kuwa katika hatua yoyote ya shauri la jinai, kabla ya kutiwa hatiani au kutolewa kwa hukumu dhidi ya mshitakiwa, DPP anaweza kumuondolea mashitaka mtuhumiwa.Hata hivyo Juni 11 mwaka huu, Chusa alitajwa katika maelezo ya shahidi mmoja na katika maelezo ya washitakiwa wawili ya kukiri kosa hilo akidaiwa kuwa ndiye aliyeelekeza kuuawa kwa Msuya.Maelezo hayo ya mashahidi 57 yalisomwa mahakamani kwa kupokezana na mawakili wa Serikali, Stella Majaliwa na Florentina Laizer, mbele ya Hakimu Mkazi wa mkoa Kilimanjaro, Munga Sabuni.Katika maelezo yake ya kukiri kosa aliyoyaandika polisi, mshitakiwa wa kwanza, Shariff Mohamed, anadaiwa kueleza kuwa Chusa ndiye alimtaka afanye kila njia kumuondoa duniani Msuya.Shariff alidai, alipomtembelea Chusa akiwa chini ya ulinzi hospitali ya Babati kwa tuhuma za mauaji ya mchimbaji mdogo, William Mushi, alidai Msuya ndiye aliyetoa pesa aunganishwe kwenye kesi ya kijana huyo.“Nilipomtembelea alininong’oneza kuwa mateso yote anayoyapata ni Erasto. Aliniomba nifanye kazi ya kumtoa roho Erasto,” amekaririwa Shariff akidaiwa kukiri kosa hilo wakati akiandikisha maelezo polisi.“Nilipomtembelea mara ya pili aliniuliza kama nimeshindwa basi nitaifanya mwenyewe akitoka. Alinisisitizia nitafute watu wa kuifanya na atanirudishia fedha akitoka,”alikaririwa Shariff.Inadaiwa Shariff alieleza kuwa Chusa alienda mbali na kumshauri amtumie mshitakiwa wa pili, Shahibu Jumanne “Mredii” ambaye alikuwa ametoka gerezani siku chache zilizopita.“Siku ya tukio mimi ndiye niliyebeba bunduki (SMG) hadi King’ori nikamkabidhi Karim (Kihundwa-mshitakiwa wa tano) niliwaambia wasichukue chochote kwani ndio maelekezo ya Chusa,”Sharif alidai.Katika maelezo hayo, Sharif amekaririwa akidai kuwa baada ya mauaji hayo alikwenda hospitalini Babati na kumjulisha Chusa kuwa tayari kazi imefanyika na alifurahi sana.Shariff ndiye ambaye pia katika maelezo ya mshitakiwa wa sita, Sadik Mohamed Jabir anadaiwa kueleza kuwa ndiye alietoa Sh4 milioni za kununua bunduki ya SMG iliyotumika katika mauaji.Shahidi mwingine, Shujaa Godfrey Baruti ambaye alikuwa msimamizi wa migodi ya Msuya, alidai katika maelezo yake kuwa Chussa na Erasto walikuwa hawaelewani kwa mwaka mzima.Katika maelezo yake, Baruti alidai Chusa alikuwa akimtuhumu Erasto kuwa alikuwa ametoa Sh8 milioni ili yeye (Chusa) aendelee kushikiliwa kwa mauaji ya mchimbaji mdogo wa madini.Mshitakiwa wa pili, Shahibu Jumanne “Mredii”, anadaiwa kukiri polisi na kueleza kuwa Julai 26 mwaka jana, alifuatwa na Sharif ambaye alimueleza kuwa kuna biashara ya kumuua Erasto.“Aliniambia kuwa Chusa analalamika kuwa Erasto anamfuatafuata kwenye biashara zake… nilimwambia mimi sitaiweza hiyo kazi labda nimtafutie watu,”alidaiwa Mredii kukiri polisi.Kwa mujibu wa maelezo hayo, Mredii anadai Shariff alimpa Sh300,000 na kumjazia mafuta fulu tenki ili aende Babati kumtafuta mshitakiwa wa saba, Ally Mussa “Majeshi” ili aifanye kazi hiyo.Hata hivyo baada ya kufika Babati na kukutana na Ally, inadaiwa katika maelezo hayo kuwa naye alidai lazima amshirikishe mshitakiwa mshitakiwa wa nne katika kesi hiyo , Jalila Zubeir Said.“Tukiwa hapo Babati alikuja mke wa Chusa tukampeleka hospitali alikolazwa Chusa. Wakati tukiondoka Chusa aliniita na kuniambia nishirikiane na Shariff kumuondoa Erasto”anadai Mredii.Mredii katika maelezo hayo anadaiwa kukiri kwa hiyari yake na kudai kuwa Chusa alimweleza sababu za kutaka Erasto auawe ni kwamba anamsumbua kimaisha pamoja na biashara zake.Hata hivyo katika maelezo yake yaliyosomwa mahakamani, Chusa amedaiwa akikanusha kutoa maagizo ya kuuawa kwa Erasto wala kushiriki kwa namna yoyote kupanga mauaji hayo.Msuya anayemiliki vitega uchumi kadhaa, aliuawa kwa kumiminiwa risasi Agosti 7 mwaka jana saa 6:30 mchana eneo la Mijohoroni wilayani Hai mkoa wa Kilimanjaro.

Habari hii ni kwa hisani ya gazeti la Jamhuri

Ripota Wetu, Moshi
Uzalishaji wa kahawa nchini, unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 48,768 msimu wa kilimo wa 2013/2014 hadi kufikia tani 62,000 msimu wa kilimo wa 2014/2015.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania(TCB),Adolf Kumburu alisema pamoja na ongezeko hilo lakini soko la ndani bado halivutii sana.
Kumburu alisema msimu wa 2013/2014, Tanzania ilizalisha tani 21,306 za kahawa aina ya Robusta na tani 27,462 za kahawa aina ya Arabika na uzalishaji huo unatarajiwa kuongezeka.
Lakini akasema msimu wa 2014/2015 unaoanza Julai mwaka huu, Tanzania inatarajia kuzalisha tani 29,500 za kahawa aina ya Robusta na tani 32,500 za kahawa aina ya Arabika.
Kwa mujibu wa Kumburu, unywaji wa kahawa hapa nchini bado uko chini na kutolea mfano wa msimu wa 2013/2014 ambapo unywaji ulikuwa asilimia 5 ya kahawa yote iliyozalishwa.
Unywaji wa kahawa nchini kwa misimu iliyotanguliwa ni asilimia 7 ( 2012/2013), asilimia 7 (2011/2012), asilimia 8 (2010/2011) na msimu wa 2009/2010, unywaji wa kahawa nchini ulikuwa ni asilimia 7.
Mkurugenzi huyo mkuu alitoa mwito maalumu kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kunywa kahawa inayozalishwa nchini ili kuinua soko la zao hilo na kuinua kipato cha wakulima.

Ripota Wetu,Moshi

Diwani wa kata moja katika wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro kwa tiketi ya chama cha Mapinduzi (CCM), anadaiwa kufumaniwa akiwa na mke wa mtu.
 
wilaya ya Moshi ina majimbo matatu ambayo ni Moshi Manispaa, Moshi Vijijini na Jimbo la Vunjo.
 
Diwani huyo (Jina na Kata tunahifadhi) alifumaniwa Jumatano iliyopita saa moja na nusu usiku katika shamba la mahindi lililopo kata ya Shirimatunda katika Manispaa ya Moshi, akiwa na mke wa rafiki yake kipenzi.
 
Habari zinadai kuwa mke aliyefumaniwa naye ni wa rafiki yake wa karibu ambaye ni mfanyabiashara na baada ya kufumaniwa, Diwani huyo alitimua mbio na kulitelekeza gari lake eneo la tukio hadi lilipoondolewa na dereva wake.
 
Tukio hilo lililowaacha vinywa wazi wakazi wa eneo la Kagera Bonite, lilitokea baada ya mke wa Diwani huyo kutonywa kuwa mumewe anakula uroda na mwanamke mmoja katika nyumba moja ya kulala wageni.
 
Hata hivyo haieleweki ilikuwaje wasimalizie shughuli zao ndani ya nyumba hiyo ya kulala wageni hadi wakaamua kwenda kwenye shamba la Mahindi lililokuwa jirani na nyumba hiyo ya kulala wageni.
 
Wakiwa shambani, huku wakiwa katika lindi la mapenzi, ndipo mke wa diwani huyo alipotokea ghafla na kumkamata hawara wa mume wake huku akipiga ukunga wa kuomba usaidizi kwa wakazi wa eneo hilo.
 
Kuona hivyo, Diwani huyo alitimua mbio na kumwacha kimada wake akiwa nusu uchi huku akiendelea kupata kichapo kutoka kwa mke wake wa ndoa.
 
Haijafahamika moto ukoje ndani ya familia ya Diwani huyo na Timu ya Blog hii itaendelea kuchimba na kukuletea zaidi ikiwamo picha za tukio hilo. Kaa mkao wa kula.
 
Mwisho
 

baadhi ya watuhumiwa wa mauaji hayo
Bunduki ya kivita aina ya Sub Machine Gun (SMG) iliyotumika kumuua mfanyabiashara tajiri wa Mirerani, Erasto Msuya, ilinunuliwa kwa Sh4 milioni nchini Kenya, Mahakama imeelezwa.
Imeelezwa pia kwamba wauaji wanne waliokwenda eneo la tukio kutekeleza mauaji hayo, walilipwa Sh5 milioni kila mmoja na washirika wao wakilipwa Sh3 milioni kila mmoja.
Hayo yamo katika maelezo ya mashahidi 57 kwa washtakiwa yalisomwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa Kilimanjaro, Munga Sabuni juzi na mawakili wa Serikali, Stella Majaliwa na Florentina Sumari waliokuwa wakipokezana kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni.
Msuya aliyekuwa anamiliki vitega uchumi kadhaa, aliuawa kwa kumiminiwa risasi Agosti 7, mwaka jana saa 6:30 mchana Mijohoroni wilayani Hai, Kilimanjaro na katika maelezo yake, mtaalamu aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, Dk Paulo Christopher alisema ulikuwa na matundu 26 ya risasi yaliyotokana na risasi 13 zilizoingia na kutokea upande wa pili zikichanachana utumbo, mapafu, ubongo na bandama.
Ushahidi huo unadai kuwa katika eneo la tukio, polisi waliokota maganda 22 ya risasi za SMG.
Mtaalamu wa makosa ya kijinai ya kompyuta, Koplo William Obeid alieleza kuwa katika kufanikisha mauaji hayo, laini mpya tano za Airtel zilisajiliwa kienyeji, zote zikiwa na jina la Motiti Ndoole na laini iliyotumika kumvuta marehemu eneo la tukio ilikuwa 0682405323.
Katika ushahidi huo, Inspekta Samwel Maimu alidai kuwa washtakiwa walikiri kosa na kueleza kuwa bunduki aina ya SMG ilinunuliwa Namanga, upande wa Kenya. Inspekta Maimu alidai kuwa mshtakiwa wa kwanza, Shariff Mohamed ndiye aliyetoa Sh4 milioni za kununua silaha hiyo na kutoa fedha za kusajili line mpya tano za simu.
Pia alidai kuwa mshtakiwa huyo, ndiye aliyetoa Sh3,350,000 zilizotumika kununulia pikipiki mbili moja aina ya Toyo na nyingine King Lion zilizotumiwa na wauaji siku ya tukio.
Katika maelezo hayo yaliyosomwa mahakamani, mshtakiwa wa kwanza (Shariff), anadaiwa kueleza namna alivyotoa maagizo ya kusajiliwa kwa line mpya.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kueleza kuwa mshtakiwa wa saba, Ally Mussa ndiye aliyemshauri atoe jiwe moja la Tanzanite litakalotumika kumshawishi marehemu Msuya. Katika maelezo hayo, ilidaiwa kuwa ndiye aliyelipa Sh4 milioni za kununua bunduki hiyo ya SMG na kwamba siku ya tukio aliibeba kwa gari lake hadi eneo la tukio na kuwakabidhi wauaji.

Katika ushahidi huo, mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa anadaiwa kueleza kuwa yeye ndiye aliyemmiminia risasi marehemu ambazo hajui idadi yake na kwamba bunduki hiyo aina ya SMG waliinunua Namanga na ilihifadhiwa nyumbani kwa Shariff sambamba na pikipiki zilizotumika.


Katika maelezo yake, mshtakiwa wa saba, Ally Mussa au Majeshi anadaiwa kueleza kuwa ndiye aliyepewa kipande cha madini na kwenda kumuuzia marehemu hotelini kwake SG Resort siku moja kabla ya mauaji.

at Thursday, June 12, 2014 Posted by Daniel Mjema 0 Comments

MAHAKAMA kuu kanda ya Moshi imewahukumu Raia wawili wa Kenya, Samweli Saitoti (Saimoo) na Michael Kimani (Mike), wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), PC Michael Milanzi mwaka 2007.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji mfawidhi wa mahakama kuu, Jaji Kakusulo Sambo alisema baada ya kusikiliza na kutafakari ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na mashahidi 18 wa upande wa Jamhuri, imeridhika kuwa Jamhuri ilifanikiwa bila kujenga kesi dhidi ya washitakiwa wote watatu bila kuacha shaka lolote.

Raia hao ambao walipambana na polisi jijini Arusha kwa saa sita wakijihami kwa silaha za kivita yakiwamo mabomu ya kurusha kwa mkono na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG), walifanya mauaji hayo yaliyoambatana na uporaji wa Sh239 milioni mali ya Benki ya NMB, Julai 11, 2007.
Pia, Jaji Kakusulo Sambo wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, amemhukumu Mtanzania, Calist Kanje kwenda jela miaka mitano kwa kuwasaidia wauaji hao wasikamatwe na polisi baada ya kufanya mauaji.
Akitoa hukumu hiyo jana, Jaji Sambo alisema upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya, Stella Majaliwa na Ignas Mwinuka, umethibitisha mashtaka hayo pasipo shaka.
Jaji Sambo alisema ushahidi wa mashahidi 18, umethibitisha kuwa raia hao wa Kenya ndiyo walioshirikiana kwa pamoja, kumuua polisi huyo ambaye taifa bado lilikuwa likihitaji utumishi wake.
“Kulikuwa na hoja ya utetezi kuwa hawakutambuliwa kikamilifu lakini PC Naftali Ashery aliyekuwa lindo na marehemu aliwatambua vilivyo wauaji hao tena kwa ukaribu,” alisema. Alisema Mahakama imeridhika kuwa maungamo waliyoyatoa mbele ya walinzi wa amani ambao ni mahakimu waliyatoa kwa hiari bila kushurutishwa.
Mahakama imeukataa utetezi wa washtakiwa hao kuwa wakati wa mauaji hawakuwa nchini, akisema ushahidi wa vinasaba (DNA), umethibitisha walikuwapo nyumbani kwa mshtakiwa Kanje.
Jaji alisema kwa kuwa washtakiwa hao walikwenda kwa Kanje na yeye akawasaidia wasikamatwe na kuwatorosha, hilo ni kosa la kusaidia wahalifu baada ya kufanya mauaji.
Jaji Sambo alisema Kanje ndiye aliyeficha gari aina ya Toyota Land Cruiser mali ya Mahakama ya Kimataifa ya Rwanda (ICTR), lililotumika katika ujambazi huo na kwamba ushahidi wa wafanyakazi wawili wa mshtakiwa huyo, unathibitisha kuwa ndiye aliyetoa maelekezo kwa dereva wake ili akalitelekeze gari hilo eneo la Uwanja wa Ndege wa KIA.
Mahakama hiyo imeamuru kiasi cha fedha, Dola 8,145 za Marekani na Sh1,769,000 walizokutwa nazo raia hao wa Kenya, zikabidhiwe Benki ya NMB, Mwanga zilikoibwa.
Washitakiwa hao, Samweli Gitau Saitoti na mwenzake Michael Kimani walitiwa hatiani kwa kosa hilo na kufungwa kwenda jela miaka 30 kila mmoja huku Mtanzania mwengine, mshitakiwa namba 10, Elizabeth Msanze "Bella", mkazi wa kwangulelo mkoani Arusha, akihukumiwa kwenda Jela miaka 7.

Wasitakiwa hao wote kwa pamoja walikuwa wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia ya askari polisi katika shauri la namba 6 ya mwaka 2011, ambapo ilidaiwa kuwa wakiwa na wenzao wengine 9, walishiriki katika tukio la uporaji na mauaji yaliyotokea, Julai 11 mwaka 2007 katika Benki ya NMB tawi la Mwanga, wilayani Mwanga , mkoani Kilimanjaro.

Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi ameuagiza uongozi wa kiwanda cha CETAWICO. Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi (PICHANI).. kuhakikisha unalipa deni la Sh700milioni unalodaiwa na wakulima wa zabibu ndani ya mwezi huu wa sita kabla Serikali haijachukua hatua nyingine. 

Zambi alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki alipotembelea wakulima wa zabibu ambao walimweleza kilio chao kuhusu deni la muda mrefu ambalo wanadai kiwanda hicho.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wa zabibu, katibu wa Ushirika wa Wakulima wa Zabibu na Masoko, Rashid Mkombozi alisema wanamdai mwekezaji huyo kwa zaidi ya miezi 9, hali inayowasababishia ugumu wa maisha kutokana na wengi wao kushindwa kulipa mikopo.

Mkombozi alisema pamoja na jitihada mbalimbali walizofanya zikiwemo kushirikisha serikali ya wilaya na mkoa ili kusaidiwa kudai madeni yao, bado wamegonga mwamba kutokana na kutopewa ushirikiano na badala yake kuishia kupewa majibu yasiyoridhisha.

Alisema siyo mara ya kwanza kwa mwekezaji huyo kutolipa madai yao kwani hata mwaka jana msimu wa mwezi wa pili ilibidi Waziri wa Kilimo, Chrisopher Chizza, aingilie kati ndiyo wakalipwa kidogo. Hivyo waliomba aondolewe kutokana na kudharau wazawa ili aletwe mwingine atakayeshirikina nao.

at Tuesday, June 10, 2014 Posted by Daniel Mjema 0 Comments

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akiwa na Dkt. Asha-Rose Migiro ( Mb) Naibu Katibu Mkuu Mstaafu na ambaye sasa ni Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wakati alipotembeleza Katibu Mkuu jana Jumatatu. Hii ni mara ya kwanza kwa Dkt. Migiro kufika Umoja wa Mataifa tangu alipostaafu Unaibu Katibu Mkuu miaka miwili iliyopita. Kabla ya Viongozi hao wawili kupiga picha hii rasmi, walikuwa na mazungumzo ya faragha ( Tete a tete). Waziri Migiro yupo hapa Umoja wa Mataifa kuhudhuria Mkutano ulioitishwa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu mchango wa Haki za Binadamu na Utawala wa Sheria katika Maendeleo Endelevu baada ya 2015.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na timu yake akiwa katika mazungumzo na Dkt. Asha- Rose Migiro ambaye alifuatana na Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi na Naibu wake, Balozi Ramadhan Mwinyi. Katika mazungumzo hayo, Katibu Mkuu alisema, Rais Jakaya Mrisho Kikwete amefanya jambo jema kumteua Dkt. Asha-Rose Migiro kwanza kuwa mbunge na kisha kumteua kuwa Waziri anayeshughulikia Sheria na Masuala ya Katiba, akasema uzoefu wake na mchango wake siyo tu kwamba ni muhimu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bali ni muhimu pia katika Jumuiya ya Kimataifa. Ban Ki Moon alishindwa kuficha hisia zake pale aliposema mbele ya Maofisa wake kwamba siku zote amekuwa akimkumbuka Asha- Rose Migiro na kwamba amefurahi sana kwamba amepata nafasi yakufika Umoja wa Mataifa.
Ban Ki Moon akiagana na Dkt. Asha-Rose Migiro baada ya mazungumzo yao.
Baada ya kuagana na Katibu Mkuu , Naibu Katibu Mkuu Mstaafu Dkt. Asha-Rose Migiro alielekea ofisini kwa Naibu Katibu Mkuu Bw. Jan Eliasson ambako nako kulikuwa na kukaribisha na tabasamu za akina yake. na kisha wakawa na mazungumzo ya faragha.Pichani ni Naibu Katibu Mkuu, Bw. Jan Eliasson akimkaribisha kwa furaha Dkt. Asha- Rose Migiro ofisi kwake kwa mazungumzo.
Wakipata picha ya pamoja.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Jan Eliasson akiwa na Dkt. Asha- Rose Migiro. Bw. Eliasson alimueleza Naibu Katibu Mkuu Mstaafu kwamba anajitahidi kufuata nyayo zake na kwamba anapenzi makubwa sana na Tanzania na Afrika kwa Ujumla, Bw. Eliasson aliwahi kufanya kazi Tanzania kama mwanadiplomasi chini ya Uongozi wa Rais wa wakati huo wa Sweden Marehemu Olof Palme.
Dkt. Asha- Rose Migiro akiagana na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliasson ( Leo jumanne ) Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba Dkt. Asha- Rose Migiro ( Mb) atakuwa miongoni wa wanajopo ( Panellist) watakaoendesha majadiliano kuhusu mchango wa haki za binadamu na utawala wa sheria katika uungaji mkono juhudi za kitaifa na kimataifa katika kuutokomeza umaskini na maendeleo endelevu. Majadiliano hayo ni sehemu ya mkutano wa siku mbili ambao umeitishwa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Bw. John Ashe na kufunguliwa na Katibu Mkuu Ban Ki Moon.Kushoto ni Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa,Balozi Tuvako Manongi
Naibu Katibu Mkuu Mstaafu akipokea shada la Maua kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wa Ofisi Binafsi ya Katibu Mkuu. Ujio wa Dkt Migiro, uliamsha shamra shamra zaina yake kutoka kwa Katibu Mkuu mwenyewe ambaye kila wakati alikuwa akiachia tabasamu pana, Baraza lake la Mawaziri pamoja na wafanyakazi wa ofisi yake Binafsi pamoja na ofisi Binafsi ya Naibu Katibu Mkuu.

at Tuesday, June 10, 2014 Posted by Daniel Mjema 0 Comments

 Mkuu wa mkoa wa Arusha  Mhe Magessa Mulongo akiangalia bidhaa zinazotengenezwa na kabila la Wahabeshi katika uzinduzi wa maonyesho ya  SIDObaadhi ya bidhaa za shanga zilizopo katika maonyesho ya sido
 Mkurugenzi wa Taha Jacqueline Mkindi akiwa anaangalia na kufurahia bidhaa zinazotengenezwaa na shanga zilizopo katika viwanja vya makumbusho katika maonyesho ya wajasiriamali toka  viwanda vidogo vidogo
 wahazabe wakiendelea kutengenez mikuki yao

 Mkurugenzi wa SIDO Taifa Omary Bakari akiwa anasoma risala kwa mgeni rasmi katika maonyesho hayo


 Meneja wa Sido  Isidori kayenze Arusha akiendelea kunogesha maonyesho hayo

at Tuesday, June 10, 2014 Posted by Daniel Mjema 0 Comments

Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Liberata Mulamula akitambulisha Mhe. Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo kwa Mkuu wa Utawala na Fedha wa Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, Mama Lily Munanka siku ya Jumatatu June 9, 2014 Waziri wa Nishati na Madini na ujumbe wake walipotembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani ulipo mtaa wa 22, jijini Washington, DC.
Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Liberata Mulamula akitambulisha Mhe. Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo kwa Rais wa Jumuiya ya Watanzania DMV, Bwn. Idd Sandaly siku ya Jumatatu June 9, 2014 Waziri wa Nishati na Madini na ujumbe wake walipotembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani ulipo mtaa wa 22, jijini Washington, DC.

Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Liberata Mulamula akitambulisha Mhe. Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo kwa Mwenyekiti wa tawi la CCM DMV, Ndugu George Sebo siku ya Jumatatu June 9, 2014 Waziri wa Nishati na Madini na ujumbe wake walipotembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani ulipo mtaa wa 22, jijini Washington, DC.
 Mkuu wa Utawala na Fedha, Mama Lily Munanka akiongea machache huku akimshukuru  Mhe. Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo na Ujumbe wake kukubali kutembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani na baadae kumkaribisha Balozi Liberata Mulamula kutoa maneno machache.
 Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Liberata Mulamula akiongea machache na kumshukuru Mhe. Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo na Ujumbe wake kwa kukubali kutembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani na baadae kumkaribisha Mhe. Waziri kuongea machache na Maafisa, na Wafanyakazi wa Ubalozi huo wakiwemo wanajumuiya.

 Mhe. Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo akiongea machache na kumshukuru Mhe. Balozi Liberata Mulamula kwa makaribisho mazuri na kuelezea sababu ya ujio wake nchini Marekani ambao alianzia New York kwenye mkutano wa  mwongo wa Nishati Endelevu kwa wote (SE4ALL) ambao Katibu  Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban   Ki Moon,  siku ya alhamisi wiki iliyopita aliuzindua rasmi   mkutano  uliohudhuriwa na  wajumbe zaidi wa  1,000 wakiwamo zaidi ya mawaziri 20 wa Nishati, wafanyabishara,  mashirika ya kimataifa yakiwamo ya fedha na  Asasi zisizokuwa za kiserikali,
Ujumbe wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huu ambao  ulianza  Juni 4 na kumalizikaJuni 6, uliongozwa na  Waziri wa  Nishani na Madini Professor   Sospeter Muhongo ambaye  pamoja na  kuhudhuria  na kuchangia mijadala mbalimbali,    ijumaa ( June 6),  alizungumza katika mkutano wa mawaziri kuhusu  nafasi ya Nishati katika  Ajenda  za Maendeleo Endelevu baada  ya 2015 na  utayari wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa Bara la Afrika kuhushu Nishati Endelevu kwa wote unaotarajiwa kufanyika mapema mwakani.
 
Picha ya pamoja ya Waheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo mwenyeji wake Balozi Liberata Mulamula.
 Waheshimiwa  Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo mwenyeji wake Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Maafisa na Wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani.
Waheshimiwa  Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo mwenyeji wake Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Ujumbe aliokuja nao Mhe. Waziri wa Nishati na Madini kutoka kushoto ni Eng.Jones Olotu(Rural Energy Agency wa Wizara ya Nishati na Madini), Eng. Rwatabangi P. Luteganya (Manager Investment TANESCO), Styden Rwebangila (Energy Engineer Wizara ya Nishati na Madini), Venosa Ngowi (Senior Petroleum Geologist TPDC), Eng. Leonard R. Masanja (Director TANESCO Board of Directors) na Eng. Yahaya I. Samamba (private Secretary to Minister Wizara ya Nishati na Madini)
Waheshimiwa  Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo mwenyeji wake Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Wanajumuiya DMV. 

*Geneviveve Nnaji na John Dumelo nao ndani

*Habib Koite, Didier Awadi kuburudisha *Filamu ya Mandela kufungua pazia

DSC_0021
Mkurugenzi Mkuu wa ZIFF, Profesa Martin Mhando (wa pili kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kuzindua rasmi Tamasha la Filamu la nchi za Majahazi la 17 maarufu kama Zanzibar International Film Festival (ZIFF). 

Kulia Msaidizi wa Kitengo cha habari ZIFF, Lara Prieston, Kushoto ni Meneja wa Tamasha la ZIFF, Daniel Nyalusi (Dean), Afisa Mawasiliano wa ZIFF, Hassan Musa "Has T" (wa pili kushoto) na Music Coordinator wa ZIFF, Edward Lusala (katikati). 
--------------------------------------------------------------------
Na Andrew Chale
DUNIA inatarajia kushuhudia tukio kubwa na la kihistoria ndani ya viunga vya Ngome Kongwe ndani Mji Mkongwe wa Stone Town, Unguja, kwa watu wa mataifa yote watakapoungana na kushuhudia ‘Hatma ya Pamoja’ (A common Destiny) Juni 14 hadi 22, 2014, katika Tamasha la Kimataifa la filamu la Zanzibar (ZIFF).

Tamasha hilo maarufu kama filamu la nchi za Majahazi ZIFF, kwa mwaka huu linatarajiwa kufanyika kwa mara ya 17, tokea kuanzishwa kwake.

Akizungumza mapema leo jijini Dar es Salaam, kwenye halfa maalum ya uzinduzi wa tamasha hilo la 17, kwa wandishi wa habari iliyofanyika Goethe Institut kituo cha utamaduni, Mkurugenzi Mkuu wa tamasha hilo, Profesa Martin Mhando, alisema tamasha hilo msimu wa mwaka huu linatarajiwa kuwa moto kwani linakuja na mambo mbalimbali yenye kuleta mabadiliko ya hali ya juu.

Ni kutokana na mabadiliko hayo, Profesa Mhando anasema tasnia ya filamu kwa Tanzania inahitaji kubadilika ikiwemo wasanii wenyewe kujituma na hata kuingia darasani ili kufanya kazi zenye uhakika.

Akimaanisha kila msanii wa filamu aweze kufikia malengo yake, hana budi kujifunza na kushirikisha wale waliotangulia katika tasnia hiyo.
Anazungumziaje kaulimbiu ya ‘A Common Destiny’

Prof. Mhando amesema kauli mbiu ya mwaka huu yenye kusema Hatma ya pamoja yenye maana ya ‘A common Destiny’, ina lengo la kuwakutanisha watu wa mataifa mbalimbali kuwa kitu kimoja na kufurahia kwa pamoja ikiwemo kubadilishana mawazo kwa pamoja kwa tasnia ya filamu, muziki, kwa mlengo ya kujenga.

“Tukiwa na haja moja, kuishi kwa amani na kuleta mapinduzi ya kiuchumi, kifikira na maendeleo kwa amani, ZIFF kwa kutumia dira hiyo hasa kupitia filamu zetu za ndani zenye mchanganyiko wa utamaduni na asili yetu.

“Wazanzibari na hata wageni watakaoshuhudia filamu hizi wataweza kuchukua utamaduni huo na kuupeleka nje kwa furaha kubwa katika kufikia hatma ya pamoja” amesema Prof. Mhando.
DSC_0082
Music Coordinator wa ZIFF, Edward Lusala akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na wasanii watakaotoa burudani kwenye tamasha hilo.
Lupita-Nyong-o-729-620x349
Lupita Nyong’o, Genevieve ndani ya nyumba

Tukio kubwa ambalo kwa sasa Tanzania hasa kwenye viunga vya Zanzibar na nchi nyingine duniani katika tamasha hilo la 17, ni ujio wa msanii wa Kenya na Mexico, Lupita Nyong’o, atakayeudhuria utoaji wa tuzo hizo za ZIFF mwaka huu.

Lupita ambaye ametwaa tuzo za Oscar na nyingine nyingi na kupelekea kutikisa Hollywood kwa sasa ni miongoni mwa mastaa watakaokuwa kwenye tamasha hilo huku akitarajiwa kuambatana na wazazi wake wote wawili pamoja na wadogo zake.

Prof. Mhando amesema tayari wazazi wote wawili wa Lupita akiwemo Dorothy na Peter Anyang’ Nyong’o, watakuwapo kwa siku zote 10 kwenye tamasha hilo huku Lupita mwenyewe akiahidi kuangalia uwezekano wa kuhudhuria japo katika utoaji wa tuzo kama ratiba za shughuli zake hazita mbana.

Prof. Mhando alisema Lupita ni zao la ZIFF na ndiyo iliyomfungulia mwanya wa kujulikana na baadaye alienda kusoma zaidi masuala hayo ya filamu, ambapo alishiriki ZIFF 2007 kama Volunteer.
Mara nyingi staa huyo amekua akihudhuria matamasha na halfa mbalimbali za utoaji wa tuzo na zawadi zingine huku akiwa ameambatana na wazazi wake wote wawili.

Lupita mbali na tuzo hiyo ya Oscar, kupitia filamu ya ‘12 Years a Slave’ pia filamu hiyo imempatia tuzo mbalimbali zikiwemo: tuzo ya Steve McQueen kama mwigizaji mwenye mvuto, mwigizaji bora wa kike aliyeshirikishwa, ‘Academy Award’, ‘Screen Actors’ Guild Award’, ‘NAACP Image Award’, ‘Independent Spirit Award’, ‘Broadcast Film Critics Association Award’, na nyingine nyingi.
Genevieve-Nnaji-Cover
Genevieve Nnaji.
Mbali na Lupita, katika kuongeza utamu wa tamasha hilo, mastaa wengine nguli wa Afrika kwa mwaka huu wanaotarajiwa kuwapo katika ushuhudiaji wa utoaji wa tuzo hizo ni pamoja na muigizaji na mwanamitindo nyota wa Nigeria, Genevieve Nnaji.
Wengine ni Amr Waked (Misri), Faouzi Bensaidi (Morocco), Nadia Buari, Richard Mote Damijo ‘RMD’, John Dumelo, Desmond Eliot na Florence Masebe.
DSC_0067
Afisa Habari wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Fizza Moloo akizungumzia kuhusiana na Filamu iliyopewa jina la "Women with Altitude" iliyoandaliwa na WFP ambapo ndani yake imeshirikisha wanawake wa kitanzania watatu waliofanikiwa kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro wakiwa wameambatana na wenzao nane kutoka Nepal na kuzungumzia changamoto mbalimbali wakati wa kupata elimu na maisha kwa ujumla itakayoonyeshwa kwenye tamasha hilo tarehe 17/6/2014 saa 19:15 jioni ukumbi wa Old Fort visiwani Zanzibar.
Filamu ya Mandela kufungua pazia

Jumla ya filamu 79, kutoka mataifa mbalimbali zinatarajiwa kuonyeshwa huku filamu iliyoingia kwenye tuzo za Oscar, ya Mandela: ‘A Long Walk to Freedom’ ndiyo itakayofungua pazia kwenye tamasha hilo, Juni 14.

“Katika filamu hizo 79 za kimataifa zitaoneshwa ZIFF, nyingi zikiwa zinatoka katika nchi za Kiafrika na filamu ya Mandela imepata bahati ya kuwa ya ufunguzi”, amesema Profesa Mhando.

Pia Profesa Mhando amesema kuwa zitakuwepo filamu zinatoka katika nchi 35 zikiwemo filamu fupi 38, filamu ndefu za kuburudisha 24 na makala 17.
DSC_0137
Meneja wa Tamasha la ZIFF, Daniel Nyalusi "Dean" akionyesha kitabu chenye ratiba nzima ya tamasha hilo litakalorindima visiwani Zanzibar kuanzia Juni 14 hadi 22 mwaka huu.

Burudani zitakazopamba

Kwa upande wake, Edward Lusala anayeshughulikia muziki kwenye tamasha hilo la 17, anasema kuwa, wamejiandaa kutoa burudani ya aina yake ambayo itaacha historia kwa mwaka huu.

Lusala amesema jumla ya makundi 18 yanatarajiwa kutumbuiza. Huku kwa wasanii gwiji wakiwemo pia Didier Awadi kutoka nchi ya Senegal na Habib Koite (Mali) wanatarajiwa kuja kuishika Zanzibar na viunga vyake.

“Wasanii Koite na Didier ni miongoni mwa wasanii wakubwa sana na wenye heshima kubwa hasa kwa muziki wao kwani wanapiga kimataifa hasa katika matamasha makubwa na wamekuwa wakipiga miziki ya kipekee. Hivyo watu wote watafurahia” amefafanua Lusala.

Ameongeza kuwa, wasanii wengine ni pamoja na Farid Kubanda ‘Fid Q’, Ambwene Yesaya ‘ Ay’, Sauti Soul, Mzungu Kichaa, Ras Inncent Nganyagwa, Grace Matata na wengine wengi ambao watatoka Tanzania.

Na kuongeza kuwa kwa sasa AY yupo nchini Malawi akijifua na moja bendi maarufu ya muziki wa Live ambapo anatajiwa kukaa jukwaani kwa zaidi ya lisaa limoja na nusu huku akiimbaLIVE.

Pia vikundi vya muziki nguli toka Tanzania, Egypt, Kenya, Uganda, Malawi na Afrika ya Kusini vitatumbuiza kila siku katika tamasha hilo.

Aidha, Lusala amesema kuwa, kwa mwaka huu wanatarajia kufanya ‘surprise’ kwa kumleta msanii mkubwa ambaye bado wapo kwenye mazungumzo na msanii huyo kutoka Afrika kusini.

Kwa upande wake Meneja wa tamasha hilo, Daniel Nyalusi amewataja wadhamini wa tamasha hilo ni pamoja mdhamini mkuu ZUKU Pay tv, huku wengine ni Ethiopian Airlines, Tanzania Media Fund TMF, ComNet, Cello, Air Uganda, Gina Din, FASTJET and United Petroleum. Wengine ni shirika la Rosa Luzemburg Foundation, Arterial Networking, Steps International, Azam marine, Prime Time Promotions, Goethe Institut na wengine wengi.

ZIFF moja kati ya matamasha ya filamu makubwa duniani hukutanisha wadau katika tasnia ya filamu. Wakiwemo waigizaji wa siku nyingi na maarufu, waongozaji, waigizaji wachanga na wanafunzi kutoka ulimwenguni kote

DSC_0119
Meneja wa Biashara wa shirika la ndege la Fastjet, Jean Uku akizungumzia udhamini wao kwenye tamasha hilo ambapo wametoa tiketi za safari ya washiriki kutoka Afrika Kusini watakaoshiriki kwenye tamasha hilo.
DSC_0084
Msanii wa Hip Hop, Harry Kaale kutoka kundi la One "The Incredible" akielezea namna watakavyotoa burudani na elimu kwa vijana kwenye tamasha hilo.
DSC_0105
Msanii Mzungu Kichaa akiwashukuru ZIFF kwa kutoa nafasi kwa wazalendo kuonyesha vipaji vyao kwenye tamasha la ZIFF.
DSC_0108
DJ maarufu Kahlil Jacobs-Fantauzzi kutoka Puerto rico akisisitiza kutoa burudani ya aina yake kwenye tamasha hilo. Picha na Zainul Mzige wa modewjiblog